Ikiwa leo ni Alhamisi, kwenye 'Tbt', tukumbushane chimbuko la muziki wa Bongofleva ambalo limekuwa likizua mijadala mara kwa mara.
Muziki huo ulianza mwanzoni mwa miaka ya 1990 ukianzia kwenye mtindo wa Hip-hop. Hapa utakumbuka wimbo wa Fid Q 'Bongo Hip-hop', anakwambia "Ulianza wewe (Hiphop) wakaja waimbaji na wabana pua (Bongofleva) wale mwewe ghafla washikaji wakatusua. Kwa kuwa wananijua mshikaji unaishi kwa miiko na zako itikadi zipo kimuziki na sio mshiko." Ni mstari wa Fid Q katika wimbo huo.
Miongoni mwa wasanii wa mwanzo wanaotajwa na wakongwe wa muziki huu ni Adili 'Nigga One' ambaye alijiunga na kundi la Kwanza Unit, baada ya kuibuka kinara katika mashindano ya kuchana'Yo! Rap Bonzanza' pamoja na Saleh Jabir ambaye anatajwa kuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki ku-rap kwa lugha ya Kiswahili. Na huo ndio ukawa mwanzo wa muziki wa Bongofleva.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 13, 2025, Dj wa muda mrefu, Nicotrack amedai muziki wa Bongofleva ulianzia maeneo ya Ilala jijini Dar es Salaam. Mwanzoni mwa miaka ya 1990.
"Kama Dj wa muda mrefu na mdau wa kiwanda cha burudani nimefanya utafiti kwa miaka mingi na kujiridhisha kuwa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongofleva ulianzia Ilala. Kwa mujibu wa utafiti nilioufanya kwa miaka kadhaa na kuchukua maoni kwa waliotutangulia, historia inasema mwanzoni mwa miaka ya 1990 waliibuka wakali Adili a.k.a Nigga One na Saleh Jabir na ndio walikuwa waasisi wa muziki huu," amesema.
Nicotrack ameendelea kusema Adili alijiunga na kundi la 'Kwanza Unit' baada ya kushinda mashindano ya kuchana 'Yo! Rap Bonanza' lakini pia Saleh Jabir aliyekuja kuwika baadaye alikuja juu baada ya kurekodi albamu yake aliyoipa jina Swahili Rap iliyokuwa na ngoma kama Ice Ice Baby, Now that we found love, Opp.
Akithibitisha muziki wa Bongofleva ulianzia Ilala, Dj Nicotrack amedai Adili 'Nigga One' na Saleh Jabir wote ni kutoka mitaa ya Ilala.
"Adili na Saleh Jabir wote ni kutoka mitaa ya Ilala na kwa mujibu wa maoni ya malegend hawa jamaa waliwika kabla hata ya Bendi ya Mawingu ya akina Dj Boni Love. Waliotamba na vibao kama Oya Msela, kabla ya GWM, Kwanza Unit, Mr II, Wagumu Weusi Asilia WWA, King Kif, The Diplomatz ya akina Saigon & Balozi Dola Soul, Mac Muga, Hard Blasters Crew na wengine wengi," amesema Dj Nicotrack.
Hata hivyo, Ilala imeendelea kuwakilishwa na wasanii wakali ambao wamekuja kuanzia miaka ya 1995 kama Imaam Abbas, Duly Sykes, Zay B, Chid Benz, Mac Dizzo, Shetta, Nuh Mziwanda na wakali wengine.

Leave a Reply