Hakuna Barakah The Prince bila Tetemesha Records!
Ni wazi kuwa Barakah The Prince ni miongoni mwa wanamuziki waliojaliwa vipaji vikubwa hasa upande wa uandishi, sauti na melodi za kuvuti zilizofanya jina lake kuwa kubwa katika Bongofleva kuanzia mwaka 2014 hadi sasa.
Tayari Barakah da Prince ameshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) na ametoa EP moja, African Prince (2018) huku mengi yakizungumzwa kuhusu mitazamo yake ila hilo haliondoi ukweli kuwa amejaliwa kipaji kikubwa. Songa nayo.
1. Kipindi anaanza muziki alitumia jina la Dogo Baraka kisha baadaye akalibadilisha na kuwa Barakah The Prince, hiyo ni sawa na rapa kutoka 26 Life, Nyandu Tozzy ambaye wakati akiwa Dar Skendo chini ya Dudu Baya alijulikana kama Dogo Hamidu.
Na katika Bongofleva wapo wengi waliofanya hivyo, mathalani kuna Maromboso kwenda Mbosso, Saraphina kwenda Phina, Lil K kwenda Young Killer, Nikki Jay kwenda Nikki Mbishi, Sarah kwenda Shaa, Dogo Shetta kwenda Shetta, Dogo Janja kwenda Janjaro n.k.
2. Wakati Young Killer akitumia jina Lil K alitoa wimbo wake, Winner (2010) uliotayarishwa na Duke Tachez na Deey Classic huku akimshirikisha Barakah The Prince ambaye wakati huo naye akitumia jina la Dogo Baraka.
Hata hivyo, siku ya kushuti video ya wimbo huo Barakah alikataliwa baada ya kupaka nywele rangi, hivyo ikabidi akaitoe na ndipo kazi ikafanyika chini Tamaduni Videos.
3. Mwaka 2013 Baraka The Prince akasainiwa Tetemesha Records chini ya Kid Bwoy ambaye alikuwa mtangazaji wa Radio Free Africa (RFA), na Kid Bwoy ndiye aliyetengeneza wimbo uliomtoa msanii huyo kimuziki, Siachani Nawe (2014).
4. Ukiachana na Baraka The Prince, Tetemesha Records imetoa wasanii wengi kutokea Kanda ya Ziwa kama Sajna, C Sir Madina, Coyo na Hussein Machozi aliyetamba na nyimbo zake kama Kafia Ghetto, Kwaajili Yako, Utaipenda, Full Shangwe n.k.
5. Hata hivyo, Barakah sio msanii wa kwanza kubadilishwa jina chini ya Tetemesha Records, kuna Hussein Machozi ambaye Kid Bwoy alilikataa jina lake la awali ndipo aliyekuwa mtangazaji mwenzake pale RFA, Fredrick Bundala ‘Sky’ akaja na hilo la Hussein Machozi.
6. Tuzo ya kwanza kwa Barakah The Prince kushinda ni kutoka TMA kama Msanii Bora Chupukizi 2015 akiwa ni msanii wa mwisho kwa kipengele hicho kutoa mshindi mmoja kwani ziliporejea msimu wa 2021 washindi wakawa wawili ila 2023 zikarejea mfumo wa awali.
Na tangu 2010 washindi wa kipengele hicho ni Diamond Platnumz (2010), Linah (2011), Ommy Dimpoz (2012), Ally Nipishe (2013), Young Killer (2014), Barakah The Prince (2015), Rapcha & Phina (2021), Kontawa & Gachi (2022) na Chino Kidd (2023).
7. Wimbo wa mwisho kwa Barakah The Prince kutoa chini ya Tetemesha Records, ni Nivumilie (2015) akishirikiana na Ruby, kwa mujibu wa Barakah, moja ya sababu ya kuachana na menejimenti hiyo ni kushindikana kufanyika kwa video ya wimbo huo.
8. Baada ya Tetemesha, Barakah alijiunga na RockStar Africa na kushiriki kuandika wimbo wa Lady Jaydee, Nasimama (2014), wakati huo wote walikuwa chini ya menejimenti hiyo ambayo sasa inawasimamia Ommy Dimpoz, Aslay, Young Lunya na Abigail Chams.
9. Barakah The Prince alikataliwa na RockStar Africa kumtumia aliyekuwa mpenzi wake Naj katika video ya wimbo wake, Nisamehe (2016) akimshirikisha Alikiba ambaye hadi sasa ndiye msanii aliyedumu na menejimenti hiyo kwa muda mrefu zaidi, miaka 10.
Hata hivyo, Barakah na Naj walikuja kufanya video ya wimbo, Marry You (2021) huku wakifungua lebo yao, Bana Music Lab (BML) ukiwa ni muunganiko wa majina yao ya awali, na hilo lilikuja baada ya msanii huyo kuachana na RockStar Africa.
10. Msanii wa kwanza kushiriki mradi wa aliyekuwa DJ wa Diamond Platnumz, RJ The DJ (Romy Jons) ambapo anashirikisha wasanii katika nyimbo zake kama anavyofanya DJ Khaled wa Marekani, ni Barakah The Prince aliyesikika katika wimbo, Bora Iwe (2018).
Leave a Reply