Mwanamuziki na mmiliki wa Lebo ya WCB Diamond Platnumz amekanusha msanii wake Mbosso kuondoka kwenye lebo hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Diamond ameeleza kuwa tayari wamekamilisha mazungumzo na Mbosso kuhusu namna nzuri ya kusimamia kazi zake hivyo kwa sasa taarifa yoyote inayozungumzia jambo hilo ipuuzwe.
"Tumekuwa na mazungumzo mazuri sana na Mbosso namna ya kuanza rasmi sasa kusimamia kazi zake na tumekamilisha jambo letu vizuri sana. Tafadhali story yoyote inayozungumzwa kuhusu jambo hili la Mbosso naomba zipuuzwe mpaka mimi binafsi na Mbosso tutakapotoa tamko rasmi," ameeleza Diamond.
Utakumbua taarifa hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa maneno yanayodai Mbosso amejing'oa kwenye lebo ya Wasafi. Stori hizo zilianza kutolewa na mmoja wa mtu wa karibu wa Diamond Platnumz, Babalevo.
Ikumbukwe Mbosso ambaye alianza safari yake ya muziki 2013 akiwa na kundi la Yamoto Band lililokuwa linaundwa na Aslay, Beka Flevour na Enock Bella alijiunga na WCB 2017 baada ya kundi la Yamoto Band kuvunjika.
Lebo ya WCB imehusika kwa kiasi kikubwa kwenye muziki wa Mbosso na kumfanya aanze kusikika kwenye nyimbo zake binafsi ambazo zimekuwa zikifanya vizuri. Tayari mkali huyu ameachia ngoma kama vile Watakubali, Sina Nyota, Kupenda, Kunguru na nyingine nyingi.
Hata hivyo, licha ya Wasafi kuendelea kukuza na kuinua vipaji vya wasanii wengi, mpaka sasa wasanii watatu wamejiondoa kwenye label hiyo ambao ni Harmonize akiwa msanii wa kwanza kusainiwa 2015 na kuondoka 2019.
Alifuata Rich Mavoko aliyejiunga na lebo hiyo 2016 na kuondoka 2018, kisha Rayvanny ambaye alisainiwa 2015 na kuaga mashindano 2022.
Leave a Reply