Kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof Palamagamba Kabudi kuhusu kuwekeza nguvu kwenye muziki wa singeli imewakosha wasanii wa muziki huo huku wakimuomba aanze na uwekezaji.
Jana Desemba 16,2024, wakati akipokelewa rasmi katika Ofisi za wizara hiyo, jijini Dodoma Pro Kabudi alisema kati ya mambo ya kuwekeza nguvu ni kuifanya dunia ijue vinyago vya kimakonde na picha za Tingatinga vinatoka Tanzania.
"Nataka tuweke nguvu kwenye muziki. Kwanza muziki huu ambao ni wa aina yake singeli, leo ikipigwa Brazil, Peru, na India ina mridimo na msisimko wa aina yake kwa wale Waafrika maelfu na mamilioni waliochukuliwa kama watumwa,"amesema.
Hata hivyo, baada ya kauli hiyo mwanamuziki na mzalishaji wa muziki wa singeli nchini Mushizo ameliambia Mwananchi kuwa kutokana na kauli hiyo ni wakati wa wasanii wa muziki huo kuongeza juhudi.
"Prof Kabudi ni kiongozi katika sekta yetu ya sanaa, kutokana na kauli yake nadhani sisi wasanii tunatakiwa kuwekeza juhudi na kuufanya muziki wa singeli kwenye umakini zaidi. Kwa sababu hadi watu wakubwa wanaona muziki katika jicho la tatu hii ni fursa yetu 1kukaza 1zaidi. Ombi langu waanze kwa kugusa kwenye uwekezaji",Mushizo.
Kwa upande wake msanii wa muziki huo na mshindi wa Tuzo za TMA mara nne Dulla Makabila amesema 1singeli ndiyo muziki unaoweza kuleta tuzo ya aina yoyote nchini.
"Ni kitu kikubwa tunashukuru kwa kutoa hilo wazo. Singeli ni utamaduni wa Tanzania na ndiyo kitambulisho na una nguvu ya kuleta tuzo yoyote kwenye hii nchi. Ni watu tu wanafanya kazi ya kudandia miziki ya watu, lakini ni kitu kikubwa ambacho hatujaamua kukiwekea nguvu na kufanya uwekezaji mkubwa. Serikali ianze kugusa wasanii wenyewe wa singeli", amesema Makabila.
Mbali na hayo msanii Imo kutoka kundi la muziki wa singeli la Wamoto linalohusisha wasichana wawili, Suzibaby na Imo, amesema kauli ya waziri huyo ni faraja kwao.
"Kauli hii ina maana kubwa kwetu kwa sababu kaangalia kwa jicho la pili. Singeli ndiyo muziki unaosumbua kwa sasa siyo Tanzania tu hata nje ya nchi, tofauti na miziki mingine.
"Naona wasanii wa singeli tungeangaliwa zaidi kwa kupewa mikopo ili tuweze kuwekeza zaidi na kuutambulisha muziki wa singeli na taifa. Wasiache kutualika kwenye majukwaa makubwa,"amesema Imo
Leave a Reply