Mastaa Watoa Neno Siku Ya Kimataifa Ya Wanawake Duniani

Mastaa Watoa Neno Siku Ya Kimataifa Ya Wanawake Duniani


Leo ni siku ya kimataifa ya wanawake ambayo huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka duniani kote kwa lengo la kutambua haraka ambazo zinalenga kupigania usawa kujinsia, haki ya kuzalisha, kupinga unyanjasaji n.k.

Je, wanawake wana ujumbe gani kwa wenzao katika siku hii muhimu kwao? hizi ni nukuu zenye hamasa kutoka kwa mastaa wa kike wenye ushawishi duniani kutoka kiwanda cha muziki, filamu, michezo na vyombo vya habari.

Oprah Winfrey

"Kitendo kikubwa cha ujasiri ambacho lazima sisi sote tufanye, ni kuwa na ujasiri wa kutoka kwenye historia yetu na ya zamani ili tuweze kuishi ndoto zetu. Fikiria kama Malkia. Malkia haogopi kushindwa, kushindwa ni hatua nyingine ya kufikia ukuu," Oprah, mtangazaji wa runinga.

Ikumbukwe baada ya kuendesha kipindi chake, The Oprah Winfrey Show kwa miaka 25, alianzisha chombo cha habari OWN mwaka 2011 na sasa utajiri wake unatajwa na Forbes kuwa ni Dola3 bilioni akiwa ndiye mwanamke tajiri zaidi kwenye tasnia ya burudani.

Asha Baraka ‘Iron Lady’
“Wanawake ni nguzo kubwa na imara, hivyo mtoto wa kike hatakiwi kuyumbishwa na chochote juu ya kuonesha uwezo wake. Ni vizuri pia kujifunza kupitia maanguko na mafanikio ya wengine katika hilo linaweza kuwa somo zuri lakini endapo tu mtoto wa kike atajiamini na kujua hakuna anayeweza kumteteresha kirahisi katika kitu anachotaka kukifikia,” Asha Baraka
Asha Baraka ni mmiliki wa kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET), amefanya makubwa katika kiwanda cha burudani.
Kupitia uongozi wake, bendi yake ya African Stars 'Twanga Pepeta' iliteka soko la burudani nchini na kuwa 'brandi' kubwa zaidi ya muziki wa dansi Tanzania.


Beyonce Knowles

"Tunahitaji kurekebisha mtazamo wetu wa jinsi tunavyojiona. Hatuna budi kujitokeza kama wanawake na kuongoza njia," Beyonce, mwanamuziki aliyevuma tangu miaka ya 1990 na kundi la Destiny's Child lilokuja kusambaratika 2006.

Akiwa ameshinda tuzo 35 za Grammy, Beyonce anapambana sana kufanya matamasha, mfano mwaka 2013/14 katika ziara yake ya dunia, The Mrs. Carter Show alifanya show 132 zilizohudhuriwa na mashabiki milioni 2.08 huku akilipwa Dola229.7 milioni.
Frida Amani
“Mwanamke yeyote anayetaka kufanya kitu namwambia siyo rahisi kufanya lakini inawezekana. Lakini kama kweli unataka kutimiza malengo nenda kwenye akili yako na uiambie hata kuwe na ugumu kiasi gani bado itawezekana.
“Lakini usiweke kwenye akili kuwa ni rahisi kwa sababu umemuona mtu fulani anakuvutia. Siyo rahisi lakini inawezekana,” Frida ameiambia Mwananchi

Frida anawakilisha wanawake katika muziki wa Hip-hop. Wengi walianza kumfahamu aliposhiriki kwenye mashindano ya kusaka vipaji ‘BSS’. Hadi sasa ametoa nyimbo kadhaa kama vile Pull Up, Tuone, Anakudanganya, Mi na We, Madame President na nyinginezo

Serena Williams

"Mafanikio ya kila mwanamke yanapaswa kuwa msukumo kwa mwingine. Tuna nguvu tunaposhangiliana," Serena, mchezaji Tenesi ambaye alistaafu Septemba 2022 na sasa ni mama watoto wawili katika ndoa yake na Alexis Ohanian.

Mwaka 2015 Serena alikuwa ndiye mwanamichezo wa kike anayelipwa fedha nyingi zaidi akichukua Dola29 milioni, na 2017 alikuwa mwanamke pekee katika orodha ya Forbes iliyotaja wanamichezo 100 wanaolipwa fedha nyingi akiwa na Dola27 milioni.

Wanswekula Zacharia 'Dora'
“Katika siku hii ya wanawake nitaendelea kuwaombea katika harakati zao za kupambana na harakati za maisha yao. Kwa sababu wanawake tunatakiwa kushikana ili kila mmoja aweze kufikia malengo yake. Mapambano ni makubwa yanahitaji umoja na ushirikiano,”
Dora ni mwigizaji na mshereheshaji nchini ameendelea kujipatia umaarufu kupitia tamthilia ya Jua Kali ambayo anacheza.

Rihanna

"Kuna kitu maalum sana juu ya mwanamke anayetawala katika ulimwengu wa mwanamume. Inahitaji neema fulani, nguvu, akili, kutokuwa na hofu, na ujasiri ili kufikia hapo," Rihanna, mwanamuziki na mfanyabiashara huku akiwa mama watoto wawili.

Akiwa umeuza rekodi zaidi ya milioni 200 duniani kote, Agosti 2021 utajiriwa wake ulikadiriwa na Forbes kufikia Dola1. 7 bilioni na kumfanya kuwa mwanamuziki wa kike tajiri zaidi duniani na wa pili baada ya Oprah Winfrey kama mburudishaji.

Feza Kessy

"Nawashauri wanawake wenzangu juu ya kujituma kufanya kazi ili kujipatia maendeleo bila kumtegemea wanaume. Naamini wenyewe tunaweza tena bila hata ya kuwezeshwa," Feza Kess, staa muziki, mitindo na filamu.

Wengi wanamkumbuka Feza kama mshiriki wa Big Brother Africa Tha Chase 2013, alifanya muziki akisainiwa na lebo kama Unity Entertainment ya AY, pia DB Records yake D'Banj kutokea Nigeria. Pia alifanya Choice FM kama mtangazaji.



Taraji P. Henson

"Mwanamke ni mpole, laini, dhaifu, na msimamo wa mwanamume ni kumlinda na kumsaidia kupanda ngazi za mafanikio. Hakikisha yuko ndani ya gari salama kwanza. Mtunze vizuri mwanamke wako, na anga ndio kikomo cha hayo yote!, Taraji P. Henson, muigizaji.

Baada ya kusomea uigizaji Chuo Kikuu cha Howard, Taraji alicheza filamu yake ya kwanza, Streetwise (1998), na tangu wakati huo amekuwa akifanya vizuri akishinda tuzo 38 na kutajwa katika orodha ya watu 100 wenye nguvu ya ushawishi duniani.

Jennifer Lopez

"Unaweza kuwa na mshauri mzuri, rafiki mzuri mwenye upendo maishani mwako ambaye hukupa ujasiri na kukufanya ujisikie vizuri juu ya mitazamo yako. Na hiyo ni nzuri sana, lakini mwisho wa siku ikiwa hujiamini, hayo yote ni sawa na bure," Lopez, muigizaji na mwanamuziki.

Filamu zake za mwanzo, Selena (1997), Anaconda (1997) na Out of Sight (1998) zilimfanya kuwa muigizaji wa Kilatini anayelipwa zaidi, kisha akatoa albamu yake, On the 6 (1999) na kuwa na mwanamke wa kwanza Marekani kushika namba moja chati ya filamu na muziki.


Mimi Mars

"Ingawa tunajua wanawake tunaiendesha hii dunia, tujaribu kusaidiana na kuwezeshana mwaka huu na hata milele. Tukatae kuchukiana, tutiane moyo na tuinue hari zetu maana kwa pamoja sisi tuna nguvu ajabu," Mimi Mars, mwanamuziki na muigizaji.

Alitoka kimuziki na kibao chake, Sugar (2017), tayari ametoa EP mbili, The Road (2018) na Christmas with Mimi Mars (2021). Katika uigizaji alifanya vizuri na thamthilia ya Jua Kali akishinda tuzo kama Tanzania Film Festival Awards, The Orange Awards n.k.

Rosa Ree

"Kwa wanawake wote wenye vipaji ni kujiamini, unatakiwa ujiamini ili uweze kukamilisha ndoto. Pili ni kuwa na imani kwenye kitu ambacho unakifanya, tatu ni kutia bidii, huwezi kuwa na ndoto halafu hutii bidii," Rosa Ree, mwanamuziki wa Hip Hop Bongo.

Huyo alitoka na nyimbo zake, One Time (2016) na Up In The Air (2017) baada ya kusainiwa The Industry, lebo ya Navy Kenzo, tayari ametoa albamu moja, Goddess (2022) huku akishinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA), The Orange Awards n.k






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags