Rais Museveni ampeleka Chameleone Marekani kutibiwa

Rais Museveni ampeleka Chameleone Marekani kutibiwa

Nyota wa muziki Uganda Joseph Mayanja 'Jose Chameleone' ambaye kwa sasa anasumbuliwa na maradhi ya kongosho, jana Desemba 23, 2024, alitolewa kwenye hospitali ya Nakasero jijini Kampala na kupelekwa nchini Marekani kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kupelekwa Marekani kwa msanii huyo kumefanywa na Waziri wa Nchi Vijana na Masuala ya Watoto nchini Uganda Balaam Barugahara, ikiwa ni agizo Rais Yoweri Museveni la kutaka msanii huyo apelekwe nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Utakumbuka kuwa taarifa za kuumwa kwa Chameleone zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita baada ya mtoto wake wa kwanza, Abba Marcus kuweka wazi kuwa baba yake anasumbuliwa na maradhi ya kongosho(Acute Pancreatitis) yaliyosababishwa na uraibu wa pombe.

"Natamani kila mmoja afahamu kuwa baba yangu hatoendelea na unywaji wa pombe. Kwa mujibu wa madaktari hatochukua miaka zaidi ya miwili kuishi kama hatoacha, hii inaniumiza sana kwa sababu huyu ndio baba yangu niliyemfahamu kwa muda wangu wa maisha," alisema Marcus kupitia video iliyokuwa ikisambaa mtandaoni.

Abba aliwataka mashabiki na marafiki wa baba yake kumpa ushirikiano ili kuimarisha afya yake na ustawi wake kwa ujumla.

"Tunatakiwa tushirikiane ili kumpa baba yangu msaada anaohitaji, nimekerwa, nina hasira sana na baba yangu kwa sababu nahisi anafanya maamuzi ya ubinafsi, nina ndugu wanne hivyo baba yangu anahitaji kuwa hai ili kunitunza mimi na ndugu zangu,” alisema Abba.

Aidha kutokana na msaada huo Chameleone amemshukuru Rais Museveni na kuwaomba watu wote wenye mapenzi mema wamuombee arudi akiwa na nguvu zote.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags