Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Moyo mjini Warsaw, Poland, umebaini kuwa ndoa huwafanya wanandoa kuwa vibonge au kuongezea uzito zaidi.
Utafiti huo uliowahusisha watu zaidi ya 2,400, ambapo wanawake na wanaume walio kwenye ndoa walionekana kuwa na hatari mara tatu ya kuwa na unene kupita kiasi ikilinganishwa na wasiooa/kuolewa.
Si Poland pekee, nchini China, utafiti uliochapishwa kwenye jarida la BMC Public Health uliowahusisha watu zaidi ya 44,000 ulibaini kuwa ndoa huongeza kwa zaidi ya asilimia 6 uwezekano wa mtu kupata uzito mkubwa. Huku sababu kubwa ikitajwa ni kupunguza kufanya mazoezi baada ya kuoa/kuolewa.
Aidha matukio kama hayo pia yameripotiwa Marekani na Australia, ambapo wataalamu wanasema mara nyingi wanandoa hujisahau mara baada ya kupata utulivu wa ndoa.
“Tunapokuwa kwenye uhusiano thabiti, hatuhisi tena shinikizo la kudumisha mwonekano. Ndiyo maana wengi huongeza kilo chache ndani ya miaka michache ya ndoa,” alisema mmoja wa watafiti.

Leave a Reply