Waliomuhoji Dogo Paten Wafungiwa

Waliomuhoji Dogo Paten Wafungiwa

 Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewazuia rasmi watangazaji wanne wa kipindi cha redio cha Genge la Gen Tok katika Kituo cha Mjini FM kilichopo jijini Dar es Salaam, kujihusisha na kazi yoyote ya kihabari kuanzia leo Julai 18, 2025, baada ya kubainika kuwa walikiuka sheria na maadili ya taaluma hiyo na kufanya kazi bila kuwa na ithibati.

Hatua hiyo imechukuliwa JAB kutokana na mahojiano yao na msanii wa Singeli, Dogo Paten, yaliyofanyika katika kipindi hicho kilichorushwa Julai 16, 2025.



Watangazaji waliokumbwa na adhabu hiyo ni Deodatha William, Mussa Mgenge, Perfect Crispin na Iddy Iddy, ambao waliendesha kipindi hicho mubashara Julai 16, 2025 na kumhoji msanii wa muziki wa Singeli anayejulikana kwa jina la Dogo Paten.

Taarifa ya kuwazuia imetolewa leo Julai 18, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa JAB, Patrick Kipangula na kueleza kuwa bodi iliwaita watangazaji hao kwa mahojiano yaliyofanyika leo, ili kupata maelezo kuhusu maudhui yaliyotangazwa.

Amesema uchambuzi wake wa kitaalamu, Bodi imebaini kuwa watangazaji hao walikiuka Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023) kwa kufanya kazi bila kuwa na Ithibati.

“ Watangazaji hao walikiuka haki ya faragha na kutweza utu wa mhojiwa kwa kumlazimisha kutoa taarifa binafsi bila ridhaa yake kinyume na Kanuni ya 11(1)(e) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji ya Redio na Televisheni), 2018 kama zilivyofanyiwa marekebisho,” amesema Kipangula.

Pia, amesema watangazaji hao walitumia lugha ya kumshushia hadhi mhojiwa kinyume na Kanuni ya 11(1)(f) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji ya Redio na Televisheni), 2018 kama zilivyofanyiwa marekebisho na Kanuni ya 16(1). ikisomwa pamoja na Jedwali la Tatu aya ya 2(b) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Maudhui ya Mtandaoni 2020.

Kutokana na makosa hayo, Bodi imewapiga marufuku watangazaji hao kufanya shughuli yoyote ya kihabari hadi watakapokidhi matakwa ya sheria, ikiwa ni pamoja na kuwa na sifa za kielimu na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.

“Bodi inatoa onyo kali kwa watu wote wanaofanya kazi za kihabari kuhakikisha kuwa wanazingatia matakwa ya Sheria kwa sababu taaluma ya habari ni mhimili muhimu wa utawala bora unaotegemea ukweli, uadilifu na heshima kwa utu wa binadamu,” amesema.
Aidha, JAB imewakumbusha wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha kuwa wanaowaajiri katika nafasi za kihabari ni watu waliothibitishwa na kusajiliwa na Bodi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags