Dj Asiyeona Anavyokimbiza Kwenye Matamasha Bongo

Dj Asiyeona Anavyokimbiza Kwenye Matamasha Bongo

Muziki unapopigwa na umati kuanza kucheza kwa furaha, si rahisi mtu kufikiria mara mbili kuhusu nani aliyesimama nyuma ya vifaa vya DJ, na punde anapogundua kuwa aliyenyuma ya vifaa hivyo haoni basi tukio hilo huwa halisahauliki.

Hii ndiyo hali ambayo watu wengi wamekutana nayo wakimshuhudia Sharifu Pinda, anayejulikana kama DJ Sharif, DJ wa kwanza kutoka Tanzania asiyeona anayekimbiza katika matamasha mbalimbali.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu chanzo cha tatizolake, alieleza kuwa alipoteza uwezo wa kuona mwaka 2012.

“Nilipoteza uwezo wa kuona mwaka 2012 kutokana na matatizo ya retina. Wazazi wangu hawakuweza kunipeleka hospitalini mapema, hivyo nililazimika kuukubali ukweli huo,” alisema Dj Sharif

Aidha aliweka wazi mara ya kwanza kugundua kipaji hicho ni mwaka 2021 akiwa kwenye mafunzo ya vitendo (field) katika kituo cha redio cha jamii Wilayani Ruangwa.

“Siku moja wenzangu hawakufika kazini, hivyo nikabaki mwenyewe studio. Nililazimika kuendesha kipindi chote pekee. Ndipo nilipojua kuwa kama nataka kufaulu kwenye utangazaji, lazima nijifunze kucheza miziki,” alieleza.

Ili kuendeleza kipaji hicho Sharif alieleza kuwa alianza kujifunza kazi ya DJ kupitia mitandao akitazama video na kuzifanyia mazoezi. Akizungumza siri ya mafanikio alieleza kuwa ipo kwenye teknolojia ambapo hutumia programu maalum ya kusoma maandishi kwenye kompyuta iitwayo NonVisual Desktop Access (NVDA).

“Programu hiyo huniongoza sehemu mbalimbali, kama kusikia majina ya nyimbo lakini zaidi ya yote, ni masikio yangu ndiyo hufanya kazi kubwa,” alisema.

Licha ya tatizo lake la kutoona lakini anaeleza kuwa amehifadhi zaidi ya nyimbo 1,000 kichwani hivyo imekuwa rahisi katika kuzichanganya na kutoa vibe kwa wasikilizaji.

“Nina nyimbo zaidi ya 1,000 kichwani. Najua namna ya kuzichanganya kulingana na midundo, hisia na hali ya wimbo. DJ asiyeona huhisi muziki kwa kina zaidi kwani sisi tunategemea sauti tu.

DJ asiyeona anakupa usahihi wa sauti kwa asilimia 100. Mchanganyiko wetu huwa umezingatia mizani, uchaguzi wa nyimbo huwa wa makusudi, na wasikilizaji wanauwezo wa kuhisi tofauti hiyo,” aliongeza.

Aidha akifunguka kuhusu changamoto ameeleza kuwa changamoto anazokumbana nazo kila mara ni kwenye programu za DJ ambazo kuna muda vipengele vinabadilika.

“Kuna wakati programu haisomi baadhi ya vipengele muhimu, hivyo imenibidi kujifunza namna ya kubadilika na kutafuta njia mbadala,” alisema.

Aliongezea kwa kueleza ndoto yake “Ningependa kuwa na vifaa vyangu. Ndoto yangu ni kuwafundisha vijana wengine wenye ulemavu wa kuona, mmoja baada ya mwingine.

“Kuna vijana wengi wasioona wenye vipaji. Wanachohitaji ni fursa. Nataka kuwasaidia kuwa DJs wa kitaalamu na kupiga muziki kwenye matamasha makubwa ndani ya Tanzania. Nataka jamii ituamini itupe nafasi. Tutaonesha uwezo wetu wa kweli,” amemalizia Dj Sharif






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags