Frida Ayapiga Teke Mapenzi, Sababu Ni Hizi

Frida Ayapiga Teke Mapenzi, Sababu Ni Hizi

Inafahamika kuwa kiwanda cha muziki wa Hip-hop Bongo kina wasanii wachache. Lakini ni gumu kuwataja  waliopo  na kuliacha jina Frida Amani, ambaye  ni miongoni mwa rapa wa kike ambao wamekuwa na mafanikio kwenye muziki huo.

Safari ya muziki ya Frida ilianza akiwa na umri wa miaka saba akishiriki katika maonesho ya vipaji vya kuimba kanisani.

Frida ambaye 2014 alifanikiwa kuachia ngoma yake ya kwanza ‘Watasubiri’, amekuwa na muendelezo mzuri hadi kuingia kwenye rekodi  ya kuwa msanii wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kutumbuiza kwenye jukwaa la Sauti za Busara  2025.

Akizungumza na Mwananchi Scoop amesema bado kiwanda cha muziki wa hip-hop nchini kinasua siyo kwa wasanii wa kike tu bali hata wa kiume

"Hiyo nadhani ni kutokana na uwekezaji ambao unawekwa kwenye muziki ni mdogo na hapo namaanisha uwekezaji wa kipesa, muda na vipaji," amesema

 

Ameongezea kuwa licha ya muziki huo kutofanya vizuri nchini, ndio muziki unaofuatiliwa kwa kiasi kikubwa duniani.

"Unaelekea mahali ambapo kuna mafanikio, sehemu ambapo unaona mafanikio yapo wazi. Kwa Marekani wameweza kuifanya rap kuendelea, mafanikio makubwa. Ukitaja wasanii wenye mafanikio kipesa na kila kitu utawataja wa Marekani,”amesema Frida

Aidha, Frida amesema anatarajia kuwa na jukwaa ambalo litasaidia kukuza muziki wa Hip-hop

"Mimi binafsi nina mradi wangu ambao nakuja nao mwezi wa tatu. Hili litakuwa ni jukwaa ambalo litasaidia kuleta marapa wapya. Kwenye hilo jukwaa watakuwa wa kike pekee kwahiyo tutaona wengi.

"Tutazunguka nchi nzima lakini kwa sasa bado ipo kwenye siri kidogo. Lakini itakuwa nchi nzima na itaangalia vipaji vya watoto wa kike ambao wanarap,”amesema

Hata hivyo Frida amesema namna ambavyo amekuwa akiyaponda mapenzi kwenye nyimbo zake ndivyo maisha yake halisi yalivyo.

 

" Kwa sasa sipo kwenye mapenzi. Nipo single, lazima nita-diss mapenzi. Mpaka atakapopatikana mpenzi, kwahiyo akija mpenzi nitaelezea uzuri wa hilo penzi lakini kwa sasa nitawaua sana wenye mapenzi yao.

"Sio kwamba sipati wanaume wenye vigezo vyangu. Nadhani ni mimi pia sipo tayari kwa sababu, nafanya kazi sana na nina mambo mengi sana. Mapenzi yanahitaji kujitoa hususani kwa mwanaume anahitaji mwanamke ambaye atampa muda wake kwa asilimia 100  kwa sasa nadhani sipo tayari kufanya hivyo,”amesema

 

Amesema kutokana na kazi zake kuwa nyingi anashindwa kujigawe kwenye mahusiano lakini akitokea mwanaume mwelewa anaweza kuwa naye.

"Mimi vitu vyangu vipo kwenye muda ambao ni sahihi. Kila ninachohitaji kitatokea kwenye maisha yangu. Kama ni mahusiano nimeishakuwa kwenye mahusiano lakini hakuna mahali yalinipeleka so for now nataka nijijenge,”amesema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags