Unaifahamu Kilwa Jazz Band, ambayo ilipoanza ilikuwa inapiga nyimbo zake kwa mitindo mbalimbali ikiwemo Rhumba, Chacha, Samba, Bolelo na kadhalika, lakini ilikuwa na sifa maalumu kwa upigaji wa chacha. Bahati mbaya katika zama hizi mitindo yote iliyotajwa imebebeshwa jina moja tu la Rhumba.
Kilwa Jazz Band ikaja kuwa moja ya bendi tishio jijini Dar es Salaam, mpaka siku hizi wengi huufahamu wimbo wa Kilwa Jazz Band wenye maneno haya;
Napenda nipate lau nafasii,
Nipate kusema nawe kidogo aah mamaa aah
Rohoni naumiaa,
Hakika lakufanya bado sijaliona,
Nimeona leo bora nikuimbee,
Huenda punde roho yako ikadundaa
Ikaja siku ukaja nipoza moyo ooh mama rohoni naumia…
Wimbo huu wa Kilwa Jazz Band, ulinakili muziki wa wimbo ulioitwa Mokoloko Nakokufa wa Bendi ya African Fiesta ya Kongo. Wimbo huu ni kati ya nyimbo za Kilwa Jazz Band ambazo zilipendwa na bado zinapendwa sana.
Licha ya wengi kuifahamu bendi hiyo kwa wimbo huo, fahamu kuwa ilishiriki katika mambo mengi makubwa ya Kitaifa.
Kilwa Jazz Band ndio iliyotumbuiza dansi maalumu la sherehe ya siku Tanganyika inapata Uhuru Desemba 09, 1961, siku hiyo iliporomosha wimbo maalumu wa kusifia Tanganyika kupata Uhuru. Wimbo huo ulikuwa na maneno haya;
“Ewe mola tunakuomba,
Uibariki nchi yetu
Tanganyika na jirani zetu,
Uhuru tumeshaupata
Lakini nyoyo zinashaka,
Wenzetu wanateseka,
Wakoloni wamewashika…”
Hata hivyo baada ya hapo Kilwa Jazz Band iliheshimika sana, iliteuliwa na serikali kushiriki sherehe za Uhuru wa Malawi na Uganda.
Wimbo wake mmoja maarufu ulitokana na maneno aliyoyatamka Mwalimu Nyerere mwisho wa hotuba yake moja, ulipata kupendwa sana. Wimbo huo ulikuwa na maneno ya Kiingereza, ‘It can be done, play your part’

Leave a Reply