Je Wajua Celine Dion Alikataa Kuimba My Heart Will Go On

Je Wajua Celine Dion Alikataa Kuimba My Heart Will Go On

Kila ifikapo siku ya Alhamisi watu hupamba mitandao ya kijamii kwa picha na video za matukio yaliyopita. Matukio hayo hugusa sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye michezo, familia na hata upande wa burudani ya muziki na filamu.

Kwa upande wa burudani ya muziki Alhamis ya leo nakurudisha nyuma kidogo kukujuza na kukusanua yale aliyowahi kuyafanya mwanamuziki kutoka Canada Celine Dion alivyokataa kuingia studio kwa ajili ya kuimba wimbo pendwa wa mashabiki na wadau wa burudani dunaini kote wa ‘My Heart Will Go On’.

Inaelezwa kuwa wakati filamu ya Titanic inakaribia kumaliziwa kurekodiwa mwaka 1997, mtayarishaji wa muziki James Horner alikuwa na ndoto ya kutengeneza wimbo wa mapenzi utakaobaki kwenye kumbukumbu za watu. Akashirikiana na mwandishi Will Jennings walitengeneza demo ya ‘My Heart Will Go On’ lakini walipomfikishia Celine Dion, alikataa kuimba wimbo huo.

Katika mahojiano yake mbalimbali Dion alisema hakuwa na hamu ya kuimba tena wimbo wa filamu kwa sababu tayari alikuwa amerekodi wimbo wa ‘Beauty and the Beast’ miaka michache nyuma na hakutaka kurudia mtindo huo.

“Sikutaka kuurekodi. Sikuupenda sana wimbo huo mwanzoni, Nilikuwa nimeshaimba ‘Beauty and the Beast’. Sikuwa na hamu tena ya kurekodi wimbo mwingine wa filamu, nilidhani kuwa ‘My Heart Will Go On’ haukuwa wimbo wangu wa lazima mimi kuingia studio,”alisema

Kutokana na hilo marehemu mume wake ambaye pia alikuwa ni meneja wake René Angélil hakushawishika kwa mara ya kwanza lakini alimuomba mke wake kujaribu kurekodi demo tu kwa ajili ya kusikiliza ambapo Dion alikubali kwa shingo upande.

“René alisema, Tufanye tu demo, mara moja. Lakini ukiona hauhitaji kufanya hivyo basi, hatutaufanya, ndipo nikakuibali, na ile demo ya kwanza ndiyo unaisikia hadi leo. Hatukuwahi kuingia studio kuirekodi tena. Wakati mwingine unapaswa kuchukua nafasi, hata kama huna uhakika,”alisema Celine

Aidha rekodi hiyo ya kwanza ya demo ndiyo iliyotumika kama toleo rasmi, ambapo wimbo huo ukawa si tu wa filamu bali pia ukawa wimbo mkubwa zaidi duniani jambo ambalo Celine mwenyewe alikiri kwamba kama asingekubali kujaribu siku ile, angepoteza moja ya mafanikio makubwa zaidi kwenye maisha yake ya muziki.

Wimbo “My Heart Will Go On” uliachiwa rasmi Desemba 3,1997 kama wimbo wa filamu ya Titanic huku ukiwahi kuongoza chati za nyimbo Marekani, Billboard Hot 100 kwa wiki mbili mfululizo, ukishika namba moja kwenye chati za nchi 20 duniani, ikiwemo Uingereza, Australia, Canada, na Ujerumani.

Lakini pia wimbo huo ulivunja rekodi ya mauzo duniani, ukiuza zaidi ya milioni 18 ya nakala, na kuwa moja ya nyimbo za filamu zilizouza zaidi katika historia. Mbali na hayo wimbo huo umenyakuwa tuzo zaidi ya 10 ikiwa ni pamoja na Tuzo ya Oscar (1998) – Wimbo Bora wa Filamu (Best Original Song), Tuzo 4 za Grammy (1999) ikiwemo Record of the Year, Song of the Year, Best Female Pop Vocal Performance, na Best Song Written for a Motion Picture na Tuzo ya Golden Globe (1998) – Wimbo Bora wa Filamu.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags