Mwanamuziki kutoka Canada, Justin Bieber ameendeleza vita yake na Paparazi (waandishi wa udaku) ambapo jioni ya jana aliandika ujumbe akionesha kutopendezwa na vitendo vya watu hao.
Kupitia mitandao ya kijamii ya hitmaker huyo wa ngoma ya 'Sorry,' aliandika kuhusu mizozo yake na paparazi akihusisha masuala ya kuwa na hasira baada ya kuzinguana na mwandishi hivi karibuni.
“Watu huwa wananiambia nipate usaidizi, Huoni kama ningeweza kujirekebisha, ningekuwa tayari nimeshafanya hivyo? Najua nimevunjika moyo. Najua nina masuala ya hasira. Nimetumia maisha yangu yote nikijaribu kuwa kama watu walivyoniambia ninahitaji kubadilika ili nifanane na wao.
Lakini hilo linanifanya nichoke na kukasirika zaidi. Kadiri ninavyojaribu kukua ndivyo ninavyojitahidi kubadilika ndivyo inavyozidi kuwa ngumu. Kadiri ninavyozidi kuzingatia. Yesu ndiye mtu pekee anayenifanya nitake kuyaelekezea maisha yangu kwa wengine. Kwa sababu kusema kweli, hivi majuzi nimechoka kujifikiria, na wewe sivyo? ,”ameandika Bieber
Bieber mwenye umri wa miaka 31 hivi karibuni alionekana ufukweni na paparazi alikuwa akimfuatilia, jambo ambalo lilimfanya apatwe na hasira na kumfukuza paparazi huyo.
Aidha baada ya tukio hilo Bieber aliomba paparazi hao kumuacha kwani ameamua kuishi maisha yake kama ambavyo binadamu wengine wanaishi bila kusumbuliwa na watu kama hao.
Hatahivyo hivi karibuni timu ya msanii huyo iliripoti kuwa na wasiwasi kuhusu afya ya akili na mwili ya Bieber huku wakisema watu wanatumia kigezo hicho kumkashifu msanii huyo.
“Ni ya kuchosha na ya kusikitisha na inaonyesha kwamba licha ya ukweli ulio wazi, watu wamedhamiria kuweka hadithi hasi, za kashfa na zenye madhara,”walisema timu yake.
Timu yake iliongeza kuwa kwasasa msanii huyo anaangazia jukumu lake kama baba kwa mwanae 'Jack Blues' pamoja na kutengeneza muziki mpya. Justin na mkewake Hailey walimkaribisha mtoto wao huyo wa kwanza mwezi Agosti, 2024.
Justin Bieber ni moja ya msanii ambaye kipaji chake kilitambulika akiwa na miaka 15 mwaka 2009 huku akitamba na ngoma kama Baby, Sorry, Never Say Never, Love Me, Yummy, One Time na nyinginezo nyingi.

Leave a Reply