Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi leo Mei 7,2025 akiwa bungeni jijini Dodoma amesema kwa mwaka 2024/25 migogoro ya wasanii imepungua.
Waziri Kabudi ambaye leo amewasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26, amesema katika kusimamia maslahi ya wasanii, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limefanya vikao vya utatuzi wa migogoro ya wasanii wa muziki kupitia Dawati la Sheria, Maadili na Usuluhishi.
"Kati ya migogoro 18 iliyopokelewa kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025, migogoro 15 ilitatuliwa na migororo mitatu (3) ipo kwenye hatua tofauti za utatuzi. Mwenendo unaonesha kwamba migogoro ya kimasilahi baina ya wadau wa sanaa 70 imekuwa inapungua kutokana na hatua ambazo Baraza kupitia Dawati hilo, imekuwa inachukua ikiwamo kutoa elimu na ushauri kwa wadau kuhusu masuala ya mikataba ya kazi za sanaa,"amesema
Hata hivyo kwa upande wa wasanii wa filamu ameongezea kwa kusema Bodi ya Filamu imeendelea kuchukua hatua stahiki za kuhakikisha wasanii wanapata haki zao.
"Katika kipindi husika, Bodi ya Filamu ilipokea na kushughulikia jumla ya malalamiko matatu kutoka kwa wadau wa sanaa. Kuwapo kwa Kamati hii kumewezesha kupungua kwa malalamiko ya wadau kutoka malalamiko 12 mwaka 2023/24 hadi malalamiko matatu mwaka 2024/25,"amesema
Amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025 jumla ya leseni 154 za uendeshaji wa shughuli za filamu na michezo ya maigizo zimetolewa.
"Katika jitihada za kuendelea kuwatambua wasanii wanaojihusisha na shughuli za Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini, Bodi imetoa vitambulisho 168 kwa wasanii hao hatua ambayo inawafanya waingie katika mfumo rasmi wa Serikali,"amesema
Ikumbukwe kuwa Bodi ya Filamu Tanzania ilianzishwa kwa Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza huku majukumu yake yakiwa ni kusimamia kazi za filamu na michezo ya kuigiza ikiwamo kuhakiki na kuzipanga katika madaraja kutoa vibali vya utayarishaji wa filamu kutoa ithibati za urasimishaji wa shughuli za filamu na michezo ya kuigiza.
Vilevile, Taasisi hiyo ina jukumu la kuratibu na kuendesha programu mbalimbali za kujenga uwezo na ujuzi wa wadau waliojiajiri/kuajiriwa katika Tasnia ya Filamu nchini
kama vile mafunzo ya muda mfupi, matamasha pamoja na tuzo.
Hata hivyo kwa upande wa BASATA majukumu yake ni kufufua na kukuza sanaa nchini, kufanya tafiti za masuala mbalimbali yahusuyo sanaa, kutoa ushauri na misaada
ya kiufundi kwa wasanii na wadau wa sanaa, kupanga na kuratibu shughuli za wasanii na wadau wanaojishughulisha na uzalishaji wa kazi za sanaa nchini na kutengeneza kanuni za kusimamia ubora wa kazi za sanaa

Leave a Reply