Hakuna ubishi kuwa Abigail Chams ni miongoni mwa wanamuziki wachache Bongo waliobarikiwa vitu vingi, ana sauti nzuri na melodi tamu, uandishi bora, anajua kupiga vyombo vya muziki bila kusahu uwezo wa kulitawala jukwaa.
Tayari Abigail Chams amewania Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), BET, huku akitoa Extended Playlist (EP) moja, 5 (2023) ambayo ilifanya vizuri hadi kutokea katika toleo la Apple Music, The Dotty Show. Mfahamu zaidi.
1. Abigail Chams alianza kujifunza kupiga piano akiwa na umri wa miaka mitano, alipofikisha miaka minane akawa amejua na violini, gitaa, ngoma na filimbi. Rasmi alianza muziki kwa kuweka kazi zake kwenye mitandao yake ya kijamii na polepole Bongofleva ikampokea.
Kati ya kazi zake za awali zilizoanza kumpa mashabiki kwenye majukwaa mbalimbali mtandaoni ni pamoja na Never Enough, I Thought, I’M Yours, Zero to 100, Real One, Reimagine n.k.
2. Baada ya kutoa wimbo wake, Reimagine (2020), Abigail Chams alipata nafasi ya kufanya kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) Tanzania kama balozi wao.
3. Abigail Chams ametokea katika video ya wimbo wa Harmonize, Furaha (2025) lakini yeye sio mwanamuziki wa kwanza wa kike Bongo kufanya hivyo kwa Harmonize, mshindi wa tuzo nne za African Entertainment Awards USA.
Mimi Mars alitokea katika video ya Harmonize ‘Mpaka Kesho’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Afro East (2020). Naye Feza Kessy katika video ‘Wote’ kutoka katika albamu ya tatu, Made For Us (2022).
4. Ilichukua miaka 10 ndipo akapatikana mwanamuziki mwingine wa kike Bongo kusainiwa na Sony Music, naye ni Abigail Chams hapo Juni 2022. Ikumbukwe Februari 2012, staa wa muziki wa Injili, Rose Muhando alisaini Sony, kisha kutoa kibao chake, Wololo (2013).
5. Abigail Chams ni mwanamuziki wa kwanza wa kike kutoka Afrika Mashariki kutajwa kuwania tuzo kubwa za muziki duniani za BET ambazo zinazoandaliwa na Black Entertainment Television (BET) tangu Juni 19, 2001 huko Marekani.
6. Huyu ni msanii wa tatu ndani ya Bongofleva kuwania BET baada ya Diamond Platnumz aliyewania mara tatu (2014, 2016 & 2021) ila bila ushindi wowote, na Rayvanny aliyeibuka mshindi 2017 akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashariki.
7. Abigail Chams ndiye mwanamuziki pekee wa kike aliyeshirikishwa katika albamu ya Young Lunya, Mbuzi (2024) ambapo amesikika katika wimbo ‘Toxic’ uliotayarishwa na Ammy Wave.
Kwa ujumla wasanii wengine walioshiriki katika albamu hiyo ni Marioo, Country Wizzy, Jay Melody, Mr. II Sugu, D Voice na Micky Singer. Pia kuna Dutchavelli (Uingereza), Khaligraph Jones (Kenya) na Jay Rox (Zambia).
8. Wimbo wake, Mee Too (2025) alioshirikiana na Harmonize kutokea Konde Music Worldwide, ndio wimbo pekee kutokea Tanzania ambao umesikilizwa mara nyingi zaidi (most streamed) katika mtandao wa Spotify kwa mwaka huu hadi sasa.
9. Video yake ambayo imeongozwa na Director Kenny, tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 19 YouTube ikiwa ni miezi mitano tangu itokea na ni video ya kwanza Tanzania iliyotoka mwaka huu kufikia namba hizo tena kwa kipindi kifupi.
10. Hadi sasa Harmonize ndiye mwanamuziki ambaye Abigail Chams kashirikiana naye mara nyingi wakitoa nyimbo kama Closer (2022), Leave Me Alone (2022), Me Too (2025) na Lala (2025) utakaokuwepo katika albamu mpya ya Harmonize.
Kwa kifupi wanaifukuzia rekodi ya Mwana FA na Lady Jaydee ambao wametoa nyimbo kama Sitoamka (2002), Wanaume Kama Mabinti (2003), Alikufa kwa Ngoma (2004), Hawajui (2005), Msiache Kuongea (2009) n.k.

Leave a Reply