Kwenye kijiji fulani alikuwepo chalii mmoja hivi kazi yake ilikuwa ni kuchunga kondoo. Anatoka nyumbani asubuhi na mamia ya kondoo na kwenda nao porini kuwalisha. Anakaa huko hadi jioni na kuwarudisha nyumbani wakiwa wameshiba vitumbo ndi ndi ndi.
Sasa chalii alikuwa ni mtu wa makuzi. Anapenda masihara. Siku moja jioni akiwa anarudi alipofika karibu na kijiji akapiga kelele “jamani! Mbwa mwitu, mbwa mwitu.” Akimaanisha kwamba amevamiwa na mbwa mwitu wanaotaka kula kondoo wake na kumdhuru na yeye.
Wanakijijiji wakasikia kelele. Kila mtu akabeba silaha. Mwenye rungu, mkuki miksa mizuna wakakimbilia porini. Kufika kule hawakukuta mbwa mwitu, bali walikuta dogo anawacheka sana, kwamba hakukuwa na mbwa mwitu alikuwa anawazingua.
Siku si nyingi chalii akafanya mchezo huohuo. Kufika huko chalii akawacheka. Siku nyingine jioni wanakijiji walipokuwa wanaendelea na mishe zao wakasikia kelele za chalii kutoka porini: “Mbwa mwitu, jamani mbwa mwitu unadhani walifanya nini? Hawakufanya chochote. Waliambiana tu “dogo ndo michezo yake, anatania.”
Jioni ikaisha. Usiku ukaingia. Familia ikaona mbona dogo harudi nyumbani ikaamua kufuatilia porini. Kufika huko ikakuta kondoo kibao wameshambuliwa na dogo naye amelala kwenye dimbwi la damu ameraruriwa na mbwa mwitu anakaribia kupoteza maisha. Kumbe bwana siku hiyo alipokuwa akipiga kelele hakuwa anatania. Ilikuwa ni kweli mbwa wamemvamia.
Alileta makuzi mara mbili tatu watu wakaacha kumzingatia na sasa kwenye matatizo ya kweli ameishia kubaki mwenyewe. Hakuna wa kumsaidia.
Natamani hadithi hii waisikie wasanii. Zuchu kaachia ngoma mpya inaitwa Amanda, lakini kabla hajaachia aliposti Insta story akiandika ‘mtu unayeanzia na A naziona simu zako kwenye simu ya mume wangu.’ Lengo likiwa ni kutengeneza taharuki ili watu wamzingatie.
Hata hivyo, sidhani kama watu walimzingatia kwa sababu wengi waliokuwa wanaongelea jambo hilo mtandaoni walionyesha wamegundua ni kiki. Na hii ni kwa sababu sio mara ya kwanza Zuchu anafanya mchezo kama huo.
Maua Sama naye juzi kati kaachia ngoma ya kuitwa I Don’t Care, lakini kabla ya kuachia aliandika kwamba anawatangazia mashabiki wake kuwa anajitoa kwenye mahusiano aliyopo sasa hivi kwa sababu yamekuwa sio chanya kwani mpenzi wake anamnyima furaha.
Baada ya siku mbili tatu akaachia wimbo. Lakini naye ni vivyo hivyo watu hawakumzingatia. Wasanii wanatakiwa wajue mbinu hii ya kutangaza kazi zao haitafanya kazi kwa sababu wameshaitumia sana, hivyo mashabiki wameacha kuizingatia.

Leave a Reply