
Muda siyo rafiki kwa Chama
Kaondoka Chama. Kwenye nyoyo za wana Simba na wana Yanga. Sio yule aliyewaendesha atakavyo kwa pasi zenye macho. Utulivu langoni kwa adui. Na kuburuza mabeki kama viroba vya mchanga.
Kwa muda mrefu ndoto ya wana Yanga. Ilikuwa kuona Chama yule akivaa uzi wao. Wakiamini uwepo wa Chama ungewapeleka nchi ya ahadi. Lakini Chama huyu siyo Chama yule.
Maestro Chama. Mwamba wa Lusaka. Lokomotivu fenti. Triple C. Pasi zilitoka kwake tu. Pale Msimbazi alikuwa na hadhi sawa sawa na Mo. Zingeheshimiwa pesa za Mo kisha akili za Chama.
Kumtazama Chama ilikuwa zaidi ya burudani. Kulikuwa na soka tamu la Simba na soka tamu la Chama. Msimbazi walimpenda. Jangwani wote walimtamani. Ilikuwa haki yake.
Kila safari ya Simba kimataifa aliibeba mgongoni kwake. Hata watangazaji walitamani kulitaja jina lake tu. Lambisha sana nyasi mabeki wa ndani na nje. Kila timu ilionja umauti kwa amkapa.
Chama ni stori fupi sana na tamu sana. Simba hawamtaki tena. Na Yanga hawamuhitaji tena. Yanga msimu mmoja umetosha kukinai huduma yake. Wakaacha aende zake. Kila kitu ni historia kwetu na kwake.
Chama liwe somo na darasa kwa wachezaji wengine. Watambue kuwa maisha ya soka ni mafupi kama ya funza. Tazama muda aliokuja Chama hapa Bongo. Na sasa hatakiwi na pande zote za timu mbili hizi kubwa.
Leo hii kina Feitoto wapo katika ubora wa juu sana. Ndo wakati wa kuweka uso wa mbuzi. Uso wa mbuzi kwenye malipo na uso wa mbuzi kwenye kujituma zaidi. Wasicheze na wowote.
Leave a Reply