Peter Akaro
Miongoni mwa nyimbo maarufu za Oliver Mtukudzi duniani ni ule uitwao 'Neria' ambao aliuandika maalumu kwa ajili ya kutumika katika filamu (Soundtrack) inayokwenda kwa jina hilo (Neria) iliyotoka mwaka 1991.
Filamu ya Neria ambayo imeandikwa na mwandishi wa riwaya, Tsitsi Dangarembga na kuongozwa na Godwin Mawuru, inahusu misukosuko ya mwanamke mmoja (Neria) katika kitongoji cha Warren Park huko Harare, Zimbabwe ambaye alimpoteza mumewe wake katika ajali.
Mwaka 1990 Neria na Patrick walikuwa ni wanandoa wenye maisha mazuri, Patrick anapofariki familia yake hutumia mila ya Washona kumnyima Neria mali na watoto wake, huku kaka mkubwa wa mumewe akitumia hiyo kamaa fursa na kurithi mali zote.
Filamu hiyo inaanza kwa kuwaonyesha Neria na Patrick wakifurahia maisha ya kisasa, wenzi hao huenda kutembelea familia yao kijijini ambako wanashawishiwa na mama yake Patrick kubaki nyumbani badala ya kukaa mjini ambapo ni mbali na familia.
Hata hivyo, Patrick anakataa wazo hilo na kusema yeye na Neria wamejenga nyumba mjini na wameamua maisha yao ni huko, kurudi mjini, gari la Patrick linaharibika kisha anatumia baiskeli kwenda kazini ndipo anagongwa na lori na kufariki dunia papo hapo!.
Ndipo Mtukudzi aliyecheza pia filamu hiyo akivaa uhusika wa Jethro, kwa sauti yake ya unyonge anatumia wimbo wake 'Neria' kujaribu kumfariji na kumtia moyo mwanamke huyo kwa kumueleza kuwa maisha yamejaa dhiki ila ajipe moyo.
“Usivunjike moyo Neria, Mungu yu pamoja nawe (Mwari anewe). Moyo wako uwe hodari, uwe hodari, Mungu yu pamoja nawe. Kifo ni wivu, hutenganisha wale walio katika upendo. Usikate tamaa dada yangu, Mungu yu pamoja nawe," anaimba Mtukudzi katika wimbo huo ulioshinda tuzo ya M-Net kama Best Soundtrack 1992.
Muigizaji wa Zimbabwe, Jesesi Mungoshi ambaye kwa mara ya kwanza alionekana katika filamu ya African Journey (1989), ndiye alicheza nafasi ya Neria kwa mafanikio makubwa.
Kwa kutambua mchango wake katika tasnia ya filamu nchini Zimbabwe, Mei 2017, Jesesi alitunukiwa tuzo ya mafanikio maishani (Lifetime Achievement) na Chuo Kikuu cha Great Zimbabwe.
Hadi sasa Neria inatajwa kama filamu iliyoingiza fedha nyingi zaidi nchini Zimbabwe kwa muda wote, zinafuata filamu nyingine maarufu kama More Time (1993), Every’s Child (1996), Flame (1996) na Yellow Card (2000).
Ikumbukwe Oliver Mtukudzi alikuwa mwimbaji maarufu wa Afro Jazz barani Afrika kutokea Zimbabwe, alifariki Januari 23, 2019 akiwa na umri wa miaka 66 huko Harare baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari.
Mtukudzi aliyeanza kutumbuiza mwaka 1977 alipojiunga na bendi ya Wagon Wheels, aliimba kwa lugha rasmi za taifa lake, Kishona, Ndebele na hata Kiingereza, huku akiupaa muziki wake mtindo wa kipekee unaojulikana kama Tuku.

Leave a Reply