Stara Thomas msanii pekee wa kike aliyepewa shavu na Mwana FA 2003

Stara Thomas msanii pekee wa kike aliyepewa shavu na Mwana FA 2003

Ni miongoni mwa waimbaji wachache wa kike walioanza kuvuma mwanzoni mwa miaka ya 2000, uandishi na sauti yake ya kuvutia vilimfanya kujizolea mashabiki na hata wasanii wenzake walivutiwa naye kwani ni mmoja ya wasanii walioshirikishwa sana. 

Ametoa albamu mbili na kushinda tuzo mbili kubwa za muziki, ameshiriki katika miradi na kampeni nyingi za kijamii kutokana na nguvu yake ya ushawishi aliyoipata kupitia kazi yake ya muziki. Huyu ndiye Stara Thomas. 

1. Baba yake hakupenda Stara Thomas awe msanii ingawa alikuwa ni mwalimu wa Sanaa, ila Stara tayari alishapenda muziki tangu mdogo akivutiwa na wasanii kama Tshala Muana, baadaye mambo yalibadilika na hata kwenda kusomea sanaa na mengi ni historia. 

2. Akiwa sekondari Stara Thomas alikuwa anafanya muziki na In Afrcan Band na baadaye alikuja kutana na  DJ Boniluv na kupata nafasi ya kurekodi Mawingu Studio kwa kipindi fulani. 

3. Kabla ya kutoka na wimbo wake, Mimi na Wewe uliomtoa kimuziki, Stara Thomas tayari alikuwa amerekodi nyimbo mbili, 'My Bad' uliokuwa katika lugha ya Kiingereza, pia kuna 'Sikia' akiwa na Marehemu Complex. 

4. Ilimchukua miaka miwili Stara Thomas kuandika wimbo wake, Mimi na Wewe, Marehemu Ruge Mutahaba ni miongoni mwa watu wa mwanzo kuusikiliza wimbo huo kabla haujatoka, Ruge alimueleza Stara kuwa ngoma hiyo itaenda kufanya vizuri na ikawa kweli. 

5. Stara Thomas ametoa albamu mbili, Nyuma Sitorudi (2000) ikiwa na wimbo maarufu, Mimi na Wewe, na Hadithi (2002) ikiwa na wimbo maarufu, Nipo kwa Ajili Yako, huku Master J, P Funk Majani na Miika Mwamba wakishiriki kwa sehemu kubwa. 

6. Tuzo ya kwanza Stara Thomas kushinda Bongo ilikuwa ni Tanzania Music Awards (TMA) 2003 kama Msanii Bora wa Kike, tuzo ya pili ya TMA ilikuwa mwaka 2010 katika kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana (Nipigie) akiwa na AT. 

7. Stara Thomas sio msanii wa kushirikisha kabisa wasanii wenzake, hii ni kutokana na aina ya muziki wake na pia kutohitaji usumbufu wakati wa kushuti video maana baadhi ya wasanii wamekuwa wakishindwa kutokea kwenye video ya nyimbo walizoshirikishwa. 

8. Kati ya nyimbo mbili pekee za Dudu Baya alizowahi kurekodi Bongo Records kwa P Funk Majani, mmoja kamshirikisha Stara Thomas, huu unaitwa 'Sikutana', utakumbuka Master J ndiye Prodyuza aliyerekodi nyimbo nyingi za Dudu Baya. 

9. Stara Thomas ndiye msanii pekee wa kike aliyeshirikishwa katika albamu ya pili ya Mwana FA, Toleo Lijalo (2003), Stara alisikika katika wimbo, Ungeniambia. 

10. Baada ya kumaliza Chuo, mwaka 2000 Stara Thomas alipata nafasi ya kuwa Mtangazaji wa East Afrika Radio, alitangaza vipindi vya burudani kama Zhuko Time, pia alifanya DJ na kusoma habari. 

Utakumbuka Ray C naye aliwahi kuwa Mtangazaji wa East Africa Radio mwaka 1997, katika kipindi chake alikuwa anampa nafasi Babu Tale kuigiza sauti (jingle) za watu maarufu kitu ambacho alikuwa anakifanya Tale hapo awali. 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags