Anupam: Sina mpango wa kujenga, nitapanga hadi nakufa

Anupam: Sina mpango wa kujenga, nitapanga hadi nakufa


Mkongwe wa filamu nchini India, Anupam Kheri amesema kuwa licha ya kuwa na fedha za kutosha, amechagua kuishi kwenye nyumba za kupanga kwa maisha yake yote.

Mkongwe huyo ambaye ametambulika kwa uigizaji wake kwa zaidi ya miaka 40 amefichua kuwa hafikirii kumiliki nyumba yake mwenyewe.

Wakati alipokuwa kwenye mahojiano na ‘The Powerful Humans’, Anupam ameeleza kuwa uamuzi wa yeye kutokununua nyumba haujatokana na tatizo la kifedha bali anaepusha migogoro ya kifamilia inayoweza kutokea baada ya kifo chake.

“Pindi mtu anapofariki au kuondoka duniani, kuna uwezekano wa kutokea mizozo kuhusu mali aliyoacha. Kwangu mimi naona kugawana pesa kuna migogoro michache zaidi.

“Nimewaona na kuzungumza na wazee, ambao wamewahi kupitia migogoro ya aina hiyo kwa kweli inasikitisha sana. Mtu mwingine amefukuzwa nje na mwanaye, mwingine analazimishwa kusaini uhamisho wa mali yake. Hivyo basi mambo na mazungumzo ya aina hii hayatokei katika nyumba yangu,” amesema Anupam.

Aidha alisisitiza kwa upande wake maisha si lazima yawe ya kifahari kwani ili kuishi inahitajika vitu vichache tu.

“Hata Gautam Buddha aliachana na utajiri wake wote na starehe ili kuishi maisha rahisi. Unahitaji vitu vichache tu maishani nyumba ya kuishi, gari, na watu mmoja au wawili wa kufanya nao kazi. Nyumba ni nyumba tu haijalishi kama ni ya kupanga au ni yako,” amesema.

Anupam Kher, ameshiriki kwenye zaidi ya filamu 500 katika lugha mbalimbali, hasa za Kihindi, Kiingereza na Kipunjabi. Baadhi ya filamu alizocheza ni Saaransh (1984), Dilwale Dulhania Le Jayenge (1995), Kuch Kuch Hota Hai (1998), Special 26 (2013), The Accidental Prime Minister (2019), Hotel Mumbai (2018 na nyinginezo.

Kupitia filamu hizo amefanikiwa kunyakua tuzo mbalimbali ikiwemo Tuzo 2 za National Film Awards, Tuzo 8 za Filmfare. Pia ametunukiwa heshima ya juu ya serikali ya India kwa mchango wake katika sanaa ikiwemo Padma Shri (2004) na Padma Bhushan (2016).

Mbali na hayo amewahi kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Filamu la India (Censor Board) na pia kufundisha katika Chuo cha Drama cha Taifa (NSD). Mpaka kufikia 2025 Anupam Kher anakadiriwa kuwa na utajiri wa takribani dola 70milioni (Sh180 bilioni) utajiri ambao ameupata kupitia malipo ya filamu, uzalishaji wa filamu, uandishi wa vitabu pamoja na kuendesha shule yake ya uigizaji.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags