Mkali wa hip-hop, Jay-Z amekuwa akiweka wazi kuhusu maisha yake ya awali na uhusiano wake na baba yake, Adnis Reeves ambaye aliikimbia familia.
Katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni, Jay-Z ameelezea jinsi baba yake alivyotoroka familia yao alipokuwa na umri wa miaka 11. Jambo ambalo liliathiri maisha yake.
“Baba yangu alikuwa mzazi mzuri sana kiasi kwamba alipotuacha, aliacha pengo kubwa. Alikuwa shujaa wangu. Barua kwa baba yangu ambayo sikuwahi kuandika. Hotuba nilizoandaa lakini sikuwahi kusema. Nilimkasirikia baba yangu kwa muda mrefu, lakini nilipokua, nilielewa mapambano yake,” amesema Jay kwenye mahojiano aliyofanya na Oprah Winfrey
Baada ya kuondoka, mama yake Jay Z, Gloria Carter alichukua jukumu la kumlea msanii huyo na ndugu zake.
Mbali na hilo wakati alipokuwa kwenye mahojiano na ‘The New York Times’ mwaka 2017, Jay-Z aliweka wazi kuwa baba yake aliacha familia baada ya kushindwa kukabiliana na msiba wa rafiki yake wa karibu, ambaye aliuawa.
"Baba yangu alikuwa mtu mwema, lakini hakujua jinsi ya kukabiliana na huzuni baada ya rafiki yake kuuawa. Alijitenga na familia na hatimaye akaondoka kabisa. Ilikuwa ni njia yake ya kukwepa maumivu, lakini kwa bahati mbaya, sisi kama familia tukawa waathirika na uamuzi huo,” alisema Jay
Hata hivyo katika albamu yake 4:44, Jay-Z alizungumza kuhusu safari ya msamaha na kuelewa sababu zilizosababisha baba yake kuondoka.

Leave a Reply