Kesi Ya Diddy Yapigwa Msasa, Mashtaka Mengine Yafutwa

Kesi Ya Diddy Yapigwa Msasa, Mashtaka Mengine Yafutwa

Waendesha mashtaka nchini Marekani wamefuta baadhi ya mashtaka dhidi ya mwanamuziki Sean “Diddy” Combs, ikiwa ni siku moja kabla ya kusikilizwa kwa hoja za mwisho pamoja na uamuzi katika kesi hiyo.

Kwa mujibu wa jarida la People, mashtaka yaliyofutwa ni pamoja na jaribio la utekaji nyara na uharibifu wa mali kwa moto (arson), ambayo yalihusishwa na madai dhidi ya Diddy kuhusu kumtishia rapa Kid Cudi. Lakini kesi nyingine kama usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya biashara ya kingono bado zinamuelemea.

Kwa kipindi cha zaidi ya wiki sita, majaji wamepata ushahidi kutoka kwa mashahidi 34, akiwemo mpenzi wa zamani wa Cpmbs, Cassie, mwanamke mwingine aliyejulikana kama Jane, wasaidizi wa karibu, pamoja na maafisa wa usalama. Mashahidi hao walieleza jinsi Combs alivyotumia umaruufu na pesa zake kuwalazimisha watu kutekeleza matukio ya kingono.

Hata hivyo upande wa utetezi (Diddy) ulihitimisha kesi yake bila kumuita shahidi yeyote, huku Diddy mwenyewe akikataa kutoa ushahidi. Badala yake, wakili wake aliwasilisha ujumbe wa maandishi kati ya Diddy na Cassie kama sehemu ya ushahidi wa utetezi.

Kesi hiyo sasa iko katika hatua ya mwisho, ambapo hoja za mwisho kutoka kwa pande zote zinatarajiwa kusikilizwa. Baraza la majaji litaanza kujadili hatima ya Diddy kuanzia Ijumaa au mwanzoni mwa wiki ijayo, hatua itakayoweka historia mpya katika maisha ya msanii huyo na tasnia ya burudani kwa ujumla.

Diddy anakabiliwa na mashtaka ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, njama ya kihalifu (racketeering), na usafirishaji kwa lengo la kushiriki katika ukahaba. Amekana mashitaka yote na endapo atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Utakumbuka Sean "Diddy" Combs alikamatwa Septemba 16, 2024 katika hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan huko Brooklyn. Kesi yake ilianza kuzikilizwa Mei 5,2025.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags