Matei Anamboka ambaye ni baba mdogo wa aliyekuwa mwigizaji wa filamu nchini, Radainus Vitalis 'Kitundu', amesema kilichoondoa uhai wa kijana wao ni maradhi ya kifua na tumbo.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 26, 2025, Matei amesema Kitundu alianza kusumbuliwa na maradhi hayo miaka miwili iliyopita lakini familia ilimuuguza hadi akarudi katika hali yake ya kawaida.
"Marehemu alikuwa anasumbuliwa sana na kifua pamoja na tumbo, hiyo hali ilianza kutokea mwaka au miaka miwili nyuma. Tukamuuguza ambavyo tunaweza na tunamshukuru Mungu kwa muda ule baada ya kumuuguza kwa miezi sita akawa yupo vizuri, akarudi katika shughuli zake," amesema Matei.
Amesema kabla ya umauti wake, hali yake ilibadilika tena wiki mbili zilizopita mpaka kupelekea kifo.
"Tukapata taarifa anaumwa kama wiki mbili kabla ya kifo chake, sisi kama familia imetushitua hatukutegemea. Kingine marehemu hakuwa mtu wa kukaa hapa nyumbani, alikuwa anaishi huko anapofanyia shughuli zake mara nyingi tulikuwa tunawasiliana naye tu.
"Lakini baadaye tulifanya udadisi tukaambiwa alikuwa anaugua kama wiki tatu alikuwa anajiuguza mwenyewe, hali ilivyomzidia akarudi kwa familia ndiyo hivyo ndani ya wiki moja baada ya kulazwa umauti ukamkuta," amesema Matei.
Kuhusu marehemu kuacha mke au mtoto, Matei amesema Kitundu hajaacha mke wala mtoto, japo aliwahi kupata mtoto akafariki.
"Marehemu tunavyofahamu hakuwa na mtoto,lakini kama kuna taarifa nyingine tupo tayari kupokea," amesema Matei.
Kitundu alifariki dunia Jumanne jioni, Juni 24, 2025, ambapo taarifa za msiba huo zilitolewa kupitia ukurasa wa Instagram wa mzalishaji na mwongozaji wa tamthilia aliyokuwa akiigiza ya ‘Jua Kali’, Leah Mwendamseka 'Lamata.'
Enzi za uhai wake, Kitundu aliigiza kwenye tamthilia ya Jua Kali kama kijana mwenye kipaji cha kucheza muziki anayetokea kwenye familia ya kimasikini. Kisha baadaye anapata nafasi ya kutoboa kimaisha lakini anashindwa kuitumia vizuri na kujikuta akirudi kwenye maisha ya kimasikini.
Muongozaji na mzalishaji mkuu wa tamthilia hiyo, Leah Mwendamseka 'Lamata' alibainisha kuwa kabla ya Kitundu kufariki, alikuwa anaumwa tangu mwaka jana na kupelekea kutoshiriki vizuri kwenye tamthilia ya Jua Kali.

Leave a Reply