Kumbe tobo la Baba Levo kimaisha lilikuwa huku

Kumbe tobo la Baba Levo kimaisha lilikuwa huku

Mungu hakupi unachotaka anakupa unachostahili! Kauli hii inajidhihirisha kwa msanii wa muziki nchini, Babalevo licha ya watu wengi kuamini kuwa mafanikio yake yanatokana na muziki anaofanya kumbe mambo ni tofauti.

Amefanya muziki kwa takribani zaidi ya miaka 20, lakini mafanikio yake makubwa ameyapata baada ya kuanza kazi ya uhamasishaji (Influencer) baada ya kutoka gerezani mwaka 2019.

Kupitia uhamasishaji wake mwaka 2024, aliweza kuibuka mshindi kama 'Best Influencer' kwenye tuzo za Ccawards Africa zilizotolewa The Super Dome, Masaki. Lakini katika muziki hajawahi kushinda tuzo yoyote ndiyo maana unaweza kusema tobo lake lilikuwa kwenye uhamasishaji.


Ambapo mpaka sasa anazungumziwa kama mmoja wa wahamasishaji wakubwa na waliofanikiwa zaidi nchini. Kabla ya Baba Levo kujikita zaidi kwenye uchawa na siasa alianza kutambulika kupitia kazi ya muziki.

Alianza kujipatia umaarufu mwanzoni mwa miaka ya 2000 enzi hizo anatambulika kama OBD katika kundi la K Town People. Aliweza kutengeneza nyimbo nyingi pendwa na kali za muda wote kabla ya kujikita zaidi kwenye uhamasishaji na siasa.

Mfano wa nyimbo ambazo ameweza kutengeneza msanii huyo na kujizolea umaarufu ni Sherehe akiwa na Queen Darling, Wanyee, Bosi Mapombe Ft Muki, Vuvuzela, Kamakawa Ft Juma Nature na nyingine nyingi.

Muziki wake uliendelea kufanya vizuri hata baada ya kuingia jela mwaka 2019 ambapo alikaa miezi mitatu na siku 22. Matatizo hayo hayakumshushia uwezo wake wa kufanya muziki.

Baada ya kutoka jela aliachia wimbo wake wa High na Low Machi 18, 2020, ngoma ambayo ilifanya vizuri na kumleta Babalevo mpya ambaye nyimbo zake zilianza kumpa mafanikio kama msanii mkubwa na kupata kolabo kutoka kwa wasanii A-listi wa Bongo Fleva.

Kuanzia mwaka 2020 Baba Levo ameweza kufanya muziki na kuachia nyimbo nyingi ikiwa ni pamoja na High na Low, Yes No, Tena, Time, Shusha Ft Diamond Platnumz, Ameen Ft Diamond Platnumz, First Time in Amerika na nyingine nyingi.

Pia ameweza kushirikishwa na wasanii kama Mbosso kwenye wimbo wa Kamseleleko, Rayvanny kwenye nyimbo kama Ngongingo. Hata hivyo, mafanikio mengi ya msanii huyo yameonekana baada ya kuingia kwenye uhamasishaji licha ya kufanya muziki kwa zaidi ya miaka 20.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags