Lamata: Sijawahi Kumuona Mwanamke Msafi Kumzidi Kajala

Lamata: Sijawahi Kumuona Mwanamke Msafi Kumzidi Kajala

Lamata Mwendamseke ‘Lamata Leah’ndilo jina lake mwongozaji na mtayarishaji wa filamu nchini ambaye ameifanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 10 hadi sasa.

Kwa kipindi chote hicho tayari ameshiriki kwenye utayarishaji wa filamu zaidi ya 40 zikiwemo, Kigodoro, Gumzo, Figo, Majuto, Shaymaa, Nesi Selena, Stella, After Death, My Princess, Tikisa, Mr & Mrs Sajuki, Poor Minds na nyingine nyingi huku akihusika kutayarisha na kuongoza Tamthilia kama Kapuni na Jua Kali.

Mbali na hizo zipo mpya Jackob's Daughter pamoja na Nafsi Yangu ambazo zinaruka kupitia Show Max. Mazungumzo kati ya Lamata na Mwananchi Scoop yalikuwa hivi…

Kutumia muda mwingi kuandaa filamu ni chanzo cha ubora wake?
" Mtu akisema miaka minne inategemea na ukubwa wa scene. Maandalizi ya muda mrefu sana siyo sababu ya kufanya kazi nzuri, kazi nzuri ni maandalizi bora," amesema Lamata.

Umewahi kununua story ya mtu ukaitumia kwenye filamu zako?
"Hapana story sijawahi kununua lakini zote ninazofanya ni za watu ndiyo maana mara zote nawagusa mashabiki. Mfano naweza kupiga story na mtu akaniambia kuhusu mpenzi wake au familia maisha yake mimi nachukua naweka kwenye kazi zangu" amesema Lamata.

Mara nyingi unaandika story muda gani?
"Muda mzuri kwangu huwa usiku. Mara nyingi na asubuhi sana. Lakini napendelea zaidi usiku unajua mchana nakuwa kwenye majukumu mengine," amesema Lamata.

Ni kweli huwa unabadilisha story juu kwa juu kwenye Jua Kali?
"Huo ndiyo uandishi, mwandishi yeyote aliye bora ni yule anayekinzana na mawazo ya watazamaji yaani kwenda kinyume na kile wanachokifikiria watazamaji.

“Hata watazamaji wakiwa wanatazama filamu kila tukio kama wanalijua hawawezi kufurahia na mimi ndiyo story zangu zile wewe unachokiwaza nakipindua ili uendelee kufuatilia" amesema Lamata

Unazingatia nini ukiwa unatafuta waigizaji wapya?
"Mimi siangalii umaarufu wa mtu naangalia sanaa yake, umaarufu sawa unakusaidia tu kwa sababu hii ni biashara, kwahiyo watazamaji wanakuwa wanamfahamu lakini hauwezi kukuta namuweka mwigizaji mbovu kwenye Juakali na hata ukimkuta hata kwa bahati mbaya basi wiki moja tu namtoa," amesema Lamata.

Ingizo jipya la Queen Masanja na Abdulrazak kwenye Juakali uliona nini kwao?
“Queen nilianza kumuona kama miaka miwili iliyopita baada ya hapo nikamuona tena kwenye kipande cha video akifanya matangazo ya nguo, niliomba kukutana nae nikamuuliza kama anapenda kuigiza. Baada ya hapo nilianza kumtengeneza kuwa mwigizaji.

"Kwa upande wa Abdul nilipomuona nikamuuliza unaweza kufanya hiki kitu na una mapenzi nacho akaniambia naweza basi nikamuweka mezani tukaongea baada ya hapo wiki ya kwanza akafanya mpaka sasa unaona yule pale," amesema Lamata.
Urafiki wako na Kajala ulianzia wapi?

“Urafiki tulianza 2014 kama siyo 2013 alipotoka jela ilitokea tu ni bahati kwa sababu yeye ni mwigizaji mimi prodjuza tukakutana kwenye kazi . Pia Wolper alituunganisha tukawa watu wa karibu.
“Kajala hapendi uchafu ni msafi kuliko chochote. Katika wanawake wasafi sijaona kama yeye. Nimekutana na marafiki wengi wa kike lakini hakuna aliyemzidi Kajala usafi yani yeye ni the best, sijawahi kukutana na mwingine hadi leo namtafuta sijaona anayemfikia,”amesema

Ipi changamoto maprodjuza wa kike kuwa wachache nchini?
"Ni uwoga ndio unatukwamisha wanawake, lakini pia kuna kukatishwa tamaa. Lamata nimeanza kupambana ili kutambulisha watayarishaji na waongozaji wa kike na mtawaona naamini kupitia mimi nitatengeneza watayarishaji wengine ," amesema Lamata.

Ipi siri waigizaji wa Lamata Village kuwa na umoja?
" Sisi tuna kauli mbiu yetu inayosema maisha ni mafupi furahia uwezavyo, hilo neno unaweza liona la starehe au burudani lakini sio kweli. Mwisho wa siku inabidi tuishi kwa sababu sisi tunafanya kazi sana usiku na mchana

“Kwaiyo lazima tupate muda kama huo lakini tunafanya kwa heshima na adabu na hiyo inanifanya nitambue shida wanazopitia waigizaji wangu najua namna gani ya kuishi nao," amesema Lamata.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags