Kwa Bongo ni nadra kukuta nyimbo za hip-hop zikipendwa na wanawake ama kuchezwa club, isipokuwa za wasanii wachache ndiyo hupata bahati hiyo.
Kati ya wasanii hao ni Moni Centrozone ambaye amefanikiwa kwa asilimia kubwa kwenye hilo, kwani nyimbo zake nyingi hasa zile zenye midondoko ya Trap zimekuwa na matokeo makubwa hadi kufikia hatua ya kupendwa na kuchezeka maeneo mbalimbali ya starehe kama Club.
Oktoba 14, 2024 Moni aliachia ngoma inayoenda kama Pisi ambayo ina miondoko ya Trap, na kuwa moja kati ya nyimbo zilizofanya vizuri hadi kuingia kwenye chati za muziki Tanzania, Kenya na Burundi.
Kubwa zaidi ngoma hiyo ilifanikiwa kumkosha Toto Bad Marioo na kuamua kumbariki kwa kutoa remix ambayo pia imeendelea kufanya vizuri tangu kuachiwa kwake.
Utaratibu wa Moni kubadilisha muziki wa hip-hop kutoka kuusikiliza magetoni mpaka kuchezeka kwenye sehemu za starehe ameufanya kwa muda mrefu sasa. Hapo awali alitoa ngoma nyingi za mtindo huo.
Mwaka 2018 aliachia Mihela ambayo ilitayarishwa na S2kizzy, ngoma hiyo imeendelea kuwa bora mpaka sasa. Agosti 22, 2019 aliachia ngoma inayoenda kama Lamoto ikiwa na midondoko hiyo.
Moni anaendelea kuwa kwenye nafasi nzuri ya muziki wa hip hop kutokana na kuamua kunyumbulika ili kuendana na muziki wa sasa. Ameshirikiana na wasanii wa Bongo Fleva kama Marioo 'Pisi', Lody Music 'Koleza', Kusah 'Chambunge' na wengine wengi.
Leave a Reply