Wengi walizoea kumuona Shufaa Lutenga 'Mama Hamisa Mobetto', katika mwili wa unene, lakini hilo limekuwa tofauti siku za hivi karibuni ambapo mwili wake unaonekana kupungua kwa kiasi kikubwa yaani unaweza kusema amekonda.
Kutokana na mabadiliko hayo ya mwili. Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakihoji nini kilichomkuta mama huyo.
Akizungumza na Mwananchi, huku akigoma kutaja kilo zake za sasa na za awali, mama huyo amesema kupungua kwa mwili wake kumetokana na kufanyiwa upasuaji nchini Uturuki kwa ajili ya kupunguza unene.
"Naona watu wengi wananishangaa mwili wangu kupungua, kila mtu anasema lake, ila hawajui kama mimi nimepunguza mwili kwa kufanya sajari, na hapa kidonda ndio kinapona, kwa sasa mwili nilionao ndiyo naupenda, kwani ule wa mwanzo ulikuwa ukinisababishia presha, miguu kuuma na uvivu wa kufanya mambo mengi.
"Nimefanya hivi sio sababu ya kufuata mkumbo wa mtu yeyote yule, bali mimi nilitaka kupunguza maradhi madogo madogo yaliyokuwa yananiandama kila uchao. Na kufanya hivi sikulazimishwa na mtu yeyote, tatizo watu wengi wanajua ukienda Uturuki au India unakuwa umeenda kwa ajili ya mtu fulani, yaani mtu kamuona mtu kafanya basi naye anaenda, hii kwangu hapana," amesema Mama Hamisa.
Amesema anafurahia alichofanya kwani ni kitu kinachompa furaha ya nafsi siku hadi siku ndiyo maana alitoa pesa kuutengenza mwili wake jinsi anavyopendezwa yeye, japo bado ana maumivu ambayo hayajapona hadi sasa sababu hana muda mrefu tangu afanye upasuaji huo.
"Kwa sasa naendelea vizuri kabisa, na hata maendeleo ya mwili wangu uko poa haswaa, ila nawashangaa watu wanaonishangaa mimi kufanya sajari katika umri huu, sasa sijui wanadhani mimi nimefanya sajari kwa kutaka urembo? Yaani binadamu ni watu wa ajabu sana, au walitaka niliendelee kuteseka na ule mwili wangu wa zamani wa unene sana?
"Hiki nilichofanya kwa wanaojua madhara ya uzito mkubwa kiafya hawawezi kunishangaa, unene ni hatari. Afya yako ni jukumu lako mwenyewe na sio la watu wengine. Mimi kama nilivyo huwa mambo ya ndani huwa napenda yabaki kuwa siri yangu, ila watu waelewe tu mimi siumwi wala sina mawazo yoyote, bali nimefanya sajari," amesema.
Kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la watu nchini kufanya 'sajari' wakiwamo wasanii na watu maarufu katika mitandao ambao wamefanya upasuaji wa kutengeneza baadhi ya viungo vyao vya mwili na wengine wakienda mbali kutaja madhara yaliyowakuta baada ya kufanya hivyo.

Leave a Reply