Huyu ndiye mtangazaji wa kwanza kutangaza Bongo Fleva redioni

Huyu ndiye mtangazaji wa kwanza kutangaza Bongo Fleva redioni

Katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali, tasnia ya burudani inaendelea kukua kwa kasi, kutokana na kuwepo kwa vyombo vingi vya habari na mitandao ya kijamii.
Lakini je umewahi kujiuliza nani ni mtangazaji wa kwanza kutangaza Bongo Fleva redioni?. Kama ulikuwa hujui basi fahamu kuwa Taji Liundi 'Master T ndiye mtangazaji wa kwanza kufanya hivyo.
Utakumbuka Taji Liundi 'Master T' ni mwasisi, mwanzilishi na mtayarishaji wa kipindi cha DJ Show cha Radio One kilichoanza kupiga nyimbo za wasanii wa ndani (Bongo Fleva), tangu mwishoni mwa miaka ya 1994, baadaye alishirikiana na mwenzake, Mike Mhagama, na hadi sasa wanatajwa kama watangazaji wenye mchango mkubwa katika kuikuza Bongo Fleva.
Hivyo basi ni ngumu kutaja maendeleo ya muziki wa Bongo Fleva bila kumtaja Taji. Hata hivyo, kutokana na mchango wake kwenye muziki huku kupitia sekta ya habari mtangazaji huyo mkongwe ametoa mtazamo wake juu ya vipindi vya burudani vya sasa kwa kusema bado kuna changamoto katika kuikuza tasnia kutokana na wengi wamejikita kusaka maudhui na sio kufanya tafiti.
"Mchango wa hivyo vipindi kwenye kuikuza tasnia, bado ni mdogo sana kwa maana vijana wengi wanatafuta maudhui na sio habari au taarifa sahihi kuhusiana na tasnia. Maudhui kwa mfano jana fulani kafanya nini?, mambo ya kibinadamu, lakini hayatazami kibiashara, kimauzo, kimapato, kifaida na uchanya wa athari zake kwa tasnia nzima," anasema.
"Tasnia ni kama kiwanda ambacho lazima kiwe na uzalishaji wa bidhaa, uuzaji, ukuzaji, promosheni, kuonekana, kusafirisha, kupatikana na kuikuza bidhaa hiyo. Na siku hizi tunazungumzia mnyororo wa thamani, yaani ni watu gani na wangapi wanahusika na bidhaa hiyo, kama uzalishaji wake ni wangapi wananufaika na kuchangia kwenye manufaa," amesema Taji.
Ameendelea kwa kusema uchambuzi wa kina wa kimkakati, si kitu ambacho unakisikia kwenye vyombo vya habari.
"Kwa mfano hii leo umuulize mtangazaji yeyote ebu nieleze thamani ya muziki wa Bongo Fleva katika soko hapa nchini kimapato, ataenda kuangalia hotuba za viongozi wachache na kupata kadirio lakini sio kamili".
"Ninavyofahamu wanaohodhi soko la Bongo Fleva ni wachache dhidi ya wengi, kwa hiyo atapima kwa wale ambao anahisi au kufanyia tathimini ya mbali kidogo. Pia kuna ambao wamejificha na wananufaika sana na muziki huu, mfano wale wenye mitandao ambayo inaruhusu watu kupakua nyimbo, na wale wanaouza kwenye DVD na Flash kwa faida yao wenyewe bila hata mhusika wa kazi yenyewe kujua," amesema.
Taji amesema vitu kama hivyo ndivyo watangazaji wanatakiwa kuvijadili kupitia vipindi vyao kwa undani bila hofu wala uwoga kwa sababu bila tasnia kutambua thamani yake halisi, basi mambo mengi yasiyo rasmi ndio yatakayotawala ambayo ndio yanaonekana sasa kama kiki na uchawa!






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags