Sanaa ya Marekani inavyowateka watu kwa namba 911

Sanaa ya Marekani inavyowateka watu kwa namba 911

Sanaa ya Marekani inavyowateka watu kwa namba 911

Usishangae ukichukua Watanzania 10 ambao hawajahi kufika Marekani hata siku moja, ukawaambia wakutajie namba ya simu ya dharura ya kupiga ukiwa Marekani, nane kati yao wakakwambia ni 911. Na Watanzania hao hao ukawaomba wakutajie namba ya dharura ya Polisi ya Tanzania wakashindwa kukwambia kuwa ni 112.

Lakini vipi nikikwambia watanzania wengi ambao wanaijua namba ya simu ya dharura ya Marekani wameifahamu kupitia sanaa, hususan filamu na video za muziki za Marekani. Mara ngapi umetazama video za muziki za Marekani umeona gari za polisi zimeandikwa 911, mara ngapi umetazama filamu za Marekani umeona mtu anavamiwa na majambazi kwenye nyumba yake anaamua kuomba msaada polisi, anapiga 911.

Lakini mara ngapi uliona kwenye filamu za Bongo mtu anahitaji msaada wa haraka polisi akapiga simu namba 112? Binafsi sijawahi kuona licha ya kuwa nimetazama video za muziki na filamu za kutosha za Bongo.

Ninachojaribu kusema ni jinsi gani sanaa ilivyo na nguvu. Jinsi gani mataifa yaliyoendelea yalifahamu nguvu ya sanaa kitambo na wakaitumia kutumezesha vitu vyao. Leo hii mtu anaweza kutazama filamu ya Marekani akajua imeshutiwa California wakati hajawahi kutia mguu hata siku moja.

Mataifa yaliyoendelea yamejua hilo kitambo. Wanafanya sanaa sio tu kuburudisha, bali pia kusambaza propaganda zao na kutangaza mataifa yao. Na kimsingi sio kitu kibaya kuwa na ubinafsi kwa ajili ya taifa lako.

Au umesahau muvi za kivita za Wamarekani na Wavietinam? Zilikuwa zinabamba ile mbaya, lakini zote zilikuwa na lengo moja kukuambia kwamba Marekani wana nguvu kuliko Wavietinam kwa sababu kwa kipindi hicho Marekani na Vietnam walikuwa wanapigana kiukweli.

Katika zile muvi masteringi wote walikuwa ni Wamerakani na maadui wote walikuwa Wavietinam. Na tukisema maadui ni maadui kwelikweli. Watu wenye roho mbaya.

Kwenye zile muvi askari wa Kivietinam walikuwa wanabaka wanawake. Wanaua watoto. Wanachoma na kuteketeza nyumba za Wavietinam wenzao. Lakini wanakuja wanajeshi wa Marekani na kuwakomboa raia wa Vietnam kwenye shida zote hizo. Masteringi wa Kimarekani wanapambana na maadui ambao ni askari wa Kivietinam na Wamarekani wanashinda.

Tena unadhani ni Wamarekani wengi basi walikuwa wanahitajika ili kushinda? Hapana. Steringi mmoja tu wa Kimarekani alikuwa anatosha kuteketeza kambi nzima ya Wavietinam. Filamu zote hizo zilikuwa na kazi moja tu ya kukufanya ukubali kuwa jeshi na taifa la Marekani sio la mchezo mchezo.

Natamani serikali ya Tanzania pia igundue hili. Labda pengine ianze kutoa pesa kwa wasanii kwa ajili ya kutengeneza kazi za aina hiyo. Kazi za kuitangaza Tanzania nje ya mipaka na ambazo zinajenga uzalendo wa ndani.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags