Wakati baadhi ya watu wakidhani anachokifanya Savanna Benson ‘Rais wa First Year’ ni maudhui tu. Mtengeneza maudhui huyo ya mtandaoni anasema kila anachokifanya kwenye mitandao kina akisi maisha yake ya uhalisia.
Savanna ambaye amekuwa akitengeneza maudhui yanayozungumzia mahusiano, ameiambia Mwananchi Scoop kuwa licha ya umaarufu wake, anapitia changamoto kwenye mahusiano kila kukicha.
"Kwanza mimi ni mtu napigwa matukio sana. Na siachani nayo mahusiano kwa sababu yananipa maudhui. Mara nyingi maudhui yangu ni maisha ya kweli naweza nikaongea kitu watu wanacheka lakini kweli kipo.
"Mimi nakuwa kwenye mahusiano na mtu wa aina yoyote, awe maarufu au asiwe. Kuna mtu maarufu alinipiga matukio, tuliachana baada ya mimi kugundua ana mwanamke mwingine. Huwezi kuniona nagombania mpenzi kwa sababu wanaume wanaaibisha,"anasema
Anasema hata yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii yakimuhusisha mwanamuziki Zuchu kurushiana maneno na aliyekuwa mpenzi wa Diamond, Rita Norbeth ni vyema wawili hao wangeachana nayo.
"Sitaki kuchagua upande wowote, lakini napenda kumwambia Zuchu anyamaze kwa sababu yule dada(Rita) sidhani kama amefikia viwango vyake. Zuchu ni mchapakazi mzuri na ana ushawishi kwa wanaweke wengi. Mwisho wa siku unagombana na mtu ambaye hana cha kupoteza,"anasema
Licha ya hayo Savanna anasema hawezi kuwa na mwanaume mwenye tabia hizi, "Siwezi kuwa na mwanaume ambaye anajiposti sana kwenye mitandao ya kijamii, utafikiri amepotea, mwanaume ambaye hajitambui, mwanaume ambaye anavaa kama mtoto anachanganya rangi. Lakini napenda mwanaume asiyeongea sana, kwa sababu mimi tayari naongea, lakini pia hela ni kigezo cha kwanza,"anasema
Utakumbuka hivi karibuni Savanna alitikisa mitandao ya kijamii baada ya kuweka wazi kuwa amenunua gari aina ya BMW
"Nilivyonunua gari baadhi ya watu wanadai nitawaonesha aliyeninunulia gari. Hiyo inaonesha jamii yetu haiamini katika mtoto wa kike na haijui nguvu ya digital. Napenda kusema Tiktok imeibua vipaji vingi sana
"Kuna ile unaingia live unapata zawadi, lakini pia imefanya vijana wengi wapate namba kwa sababu ni mtandao ambao ni rahisi kufanya hivyo ni tofauti na Instagram ambapo mpaka ufanye kitu ndiyo watu wajue. Vitu ambavyo mtu anatakiwa kuwa navyo ili awe mtengeneza maudhui ni kamera nzuri, simu yenye uwezo wa kurekodi vizuri, confidence na ubunifu,"anasema

Leave a Reply