Kampuni ya Netflix imeweka historia nyingine kupitia msimu wa tatu wa tamthilia maarufu ya Kikorea, Squid Game, baada ya sehemu hiyo kuvunja rekodi ya watazamaji katika siku tatu za mwanzo tangu kuachiwa kwake Juni 27,2025.
Katika taarifa iliyotolewa na Netflix mapema wiki hii, Squid Game Season 3 imetazamwa na zaidi ya watu milioni 61.1 ndani ya siku tatu pekee jambo ambalo halijawahi kufikiwa na tamthilia yoyote ya lugha ya kigeni kwenye jukwaa hilo.
Rekodi hii mpya imeipiku ile ya msimu wa pili wa ‘Squid Game’ na pia inaifanya tamthilia hiyo kuwa moja ya maudhui yanayoongoza katika historia ya burudani ya kidijitali.
Msimu huu wa tatu umeendelea kuweka rekodi mbalimbali ikiwa ni pamoja kuongeza zaidi ya milioni 2 ya watumiaji wapya wa Netflix ndani ya wiki moja huku ikitrend kwenye nchi zaidi ya 70 ikiwemo Marekani, Korea Kusini, Nigeria, Brazil, Ufaransa na nyinginezo.
Aidha mchambuzi wa masoko ya kidijitali, Ji-Hyun Park, amesema mafanikio haya ni ushahidi kwamba ulimwengu una kiu ya maudhui yenye ubunifu.
“Watu wanapenda tamthilia zinazochambua maisha halisi kwa lugha ya kisanii, Squid Game inaleta ujumbe mzito kuhusu mfumo wa kijamii kwa njia isiyo ya kawaida," alisema Ji-Hyun.
Misimu yote iliyopita ya Squid Game imeingia kwenye Orodha ya Top 10 ya maudhui yasiyo ya Kiingereza yanayotazamwa zaidi Netflix ambapo Msimu wa 2 ukishika namba 3 ukiwa na watazamaji milioni 2.8 na Msimu wa 1 ukawa namba 6 watazamaji milioni 1.7, jambo ambalo limethibitisha kuwa kazi za mtayarishaji Hwang Dong-hyuk ni miongoni mwa tamthilia bora zaidi duniani.
Utakumbuka msimu wa kwanza wa Squid Game ambao uliachiwa rasmi Septemba 17,2021 uliweka rekodi kushinda tuzo sita za Primetime Emmy. Ikiwemo tuzo ya kihistoria kwa mkurugenzi Hwang Dong-hyuk, ambaye alishinda tuzo ya Outstanding Directing kwa Drama Series. Waigizaji Lee Jung-jae na Lee You-mi pia walishinda tuzo kwa ufanisi wao.
Aidha msimu wa pili wa Squid Game uliachiwa rasmi Desemba 26, 2024 ukinogeshwa na mastaa kama Lee Jung-jae, Lee Byung-hun, Wi Ha-jun, na Gong Yoo. Huku kukiwa na washiriki wapya kama Yim Si-wan, Kang Ha-neul, Park Gyu-young, Lee Jin-uk, Park Sung-hoon, Yang Dong-geun, Kang Ae-sim, Lee David, Choi Seung-hyun, Roh Jae-won, Jo Yu-ri, na Won Ji-an.

Leave a Reply