Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, amesema yuko tayari kuangalia ukweli wa kesi inayomkabili msanii wa muziki Sean "Diddy" Combs, ambaye kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono pamoja na uhalifu wa kupanga (racketeering) katika Mahakama ya Shirikisho ya New York.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana, Mei 30, 2025, Trump ameeleza kuwa hajapokea ombi rasmi la msamaha kutoka kwa Diddy, lakini yuko tayari kufanyia kazi suala hilo ikiwa ataona msanii huyo ametendewa isivyo haki bila kujali uhusiano wao wa zamani wa urafiki ambao ulivunjika alipokuwa rais.
“Sijamwona, sijazungumza naye kwa miaka mingi. Sijui mengi kuhusu hilo. Nimeona mambo machache. Ningependa kuangalia ukweli wa mambo. Nikiona mtu ametendewa isivyo haki, haijalishi kama ananipenda au hanipendi,” alisema Trump.
Hata hivyo, maafisa wa karibu na Trump wamesema kuwa kutoa msamaha kwa Diddy kunaweza kuwa na changamoto, kutokana na uzito wa mashtaka yanayomkabili msanii huyo.
Kesi ya Diddy ilianza kusikilizwa Mei 5, 2025, huku kukiwa na mashahidi mbalimbali wakidai kupigwa na kushambuliwa kingono lakini Combs amekana mashtaka yote na anasisitiza kuwa vitendo vyake havikufikia kiwango cha uhalifu wa usafirishaji wa binadamu.
Hadi kufikia sasa, zaidi ya mashahidi 10 wamewasilisha ushahidi katika kesi hiyo ya shirikisho, akiwemo mpenzi wake wa zamani Cassie Ventura, msanii Kid Cudi (Scott Mescudi), aliyekuwa msaidizi wake Capricorn Clark, msaidizi wa zamani anayejulikana kwa jina la bandia Mia, pamoja na wengine.

Leave a Reply