Usiyoyafahamu kuhusu binti wa Tesa anayeendeleza alipoishia mama yake

Usiyoyafahamu kuhusu binti wa Tesa anayeendeleza alipoishia mama yake

Unaweza kusema ni furaha na huzuni kwa mashabiki wa marehemu Grace Mpunda ‘Tesa’ aliyekuwa akiigiza tamthilia ya Huba. Huzini hiyo ni kutokana na mashabiki wake kumkumbuka mwigizaji huyo aliyejua kuuvaa uhusika.
Lakini faraha hiyo ni baada ya mtoto wa marehemu huyo kuingia rasmi kwenye uigizaji huku akicheza kwenye tamthilia ya Huba aliyokuwa akicheza mama yake.

Happiness Ally ndilo jina la mtoto huyo wa kwanza wa Grace Mapunda kati ya watoto wake wawili. Akizungumza na Mwananchi anasema aliwahi kuigiza zamani lakini hakuendelea badala yake mama yake ndiyo aliendelea kufanya sanaa hiyo.

"Mwaka huu Aprili ndiyo nikarudi tena rasmi. Kuna kikundi mtaani kwetu zamani watu walinifuata nikiwa mdogo niigize. Baba yetu amefariki muda mrefu kwa hiyo tumeishi na mama kuna baadhi ya vitu nilikuwa siwezi kufanya bila yeye. Nikabidi nimshawishi na yeye kuigiza lakini hakuwa anajua wala anayataka.

"Nikamwambia akanisaidie kuwa mdhamini kwenye kundi, nilikuwa najua nampeleka kwenye interview. Tulipofika mama yangu aliambiwa afanye kitu bila kujua kama ni interview akaja kuambiwa ameshinda tangu hapo mama yangu aliingia kwenye uigizaji," anasema

Anasema anadhani ni Mungu ndiyo alitaka mama yake aanze kuingia kwenye tasnia hiyo. Kwani baada ya hapo yeye hakupenda tena kuigiza akaendelea na masomo na baadaye biashara zake.

"Ilikuwa ikitokea scene za ujana wake, alikuwa anatumia nguvu kunishawishi niigize. Nilikuwa nazicheza lakini kwakulazimishana sana,"anasema


Anasema mama yake alipofariki mzalishaji na mwongozaji wa tamthilia ya Huba Aziz Mohamed alipendekeza mmoja kutoka kwenye familia ya Grace aendeleze kufanya alichokuwa akifanya marehemu huyo ndipo Happy akarudi tena kwenye uigizaji.

"Kwa sasa kuna mabadiliko makubwa sana kwenye kiwanda cha filamu. Kipindi namuingiza mama walikuwa hawalipwi na hakukuwa na dalili kwamba wataweza kulipwa. Ilikuwa stesheni chache sana wanatoa tu chakula au Sh 4000-5000.

"Lakini siku hizi wasanii wanalipwa vizuri mfano mama yangu angekuwa ameingia kwenye sanaa kipindi hichi. Kwa jinsi ambavyo amecheza scene nyingi basi angekuwa na hela nyingi ukilinganisha na filamu alizocheza kipindi kile,"anasema

Anasema mama yake alikuwa na kipaji kikubwa hivyo alivutiwa na kazi zake. Huku akiitaja filamu iitwayo 'Fake Smile' kama pendwa kwake.

"Alicheza sana mule, lakini pia ile ndiyo movie iliyomtambulisha kwenye ulimwengu wa filamu. Alikuwa akicheza ukali nafurahi kwa sababu nyumbani mama alikuwa mkali sana nilikuwa naona anacheza uhalisia wake. Kingine alikuwa akicheza analia nilikuwa nafurahi zaidi kwa sababu ilikuwa kitu kinachomtambulisha,"anasema

Happy ambaye kwa sasa anacheza tamthilia ya Huba anasema scene ambayo ilimpa ugumu kwenye tamthilia hiyo ni wakati akiwapa taarifa wakina Tima na mashabiki kuwa Grace hayupo tena duniani.

"Niliumia kwa sababu hatunaye tena duniani. Tulicheza uhalisia wa maisha ya ukweli na mimi ndiyo muhusika wa hilo jambo, ni ngumu sana kwa sababu naona waliokuwa wanacheza naye alafu natakiwa niwaambia kuwa Tesa kafariki. Hata mimi nikijiangalia nilikuwa nahisi kulia nikaumia tena kweli,"anasema

Licha ya kuonekana katika uhusika huo Happy anasema hata apewe dau nono kiasi gani hatoweza kucheza uhusika huu

"Sanaa ni kazi ngumu sana kukivaa kitu ambacho siyo cha kweli kiwe cha kweli. Lakini siwezi kucheza scene za utupu au kuwekwa kwenye jeneza. Nitaweza kucheza nimekufa lakini siyo kuwekwa kabisa kwenye jeneza, watafute mtu mwingine au mdoli. Jeneza ni kitu cha misho zaidi kukifikirika maishani. Jeneza linaondoa watu tusiwaone tena duniani na hatujui tutawaona wapi," anasema

Anasema maisha ya umaarufu yana tabu yake lakini kwake haimpi shida kwani amejifunza vingi kutoka kwa mama yake.

"Umaarufu una changamoto kwa sababu kama ulizoea kwenda Kariakoo itabidi uende Mlimani City. Tanzania kuna baadhi ya watu wanaamini msanii yeyote ni tajiri wakati ile ni kazi kama kazi nyingine. Watu wanavyokuangalia wakikuona Kariakoo wanasema wamekuona unazagaa. Inabidi uishi maisha ambayo siyo yako inaumiza.

"Mimi kwangu hainiumizi ni kitu ambacho kilikuwepo kwenye familia. Nilimuona mama yangu naona niishi vipi. Mashabiki zangu napenda kuwaambia wanisapoti sana kama walivyokuwa wakifanya kwa mama yangu hata kama kuna vitu vimepungua nawaahidi kwamba sitawaangusha kwenye kazi yangu nitakuwa mbunifu,"anamalizia

Utakumbuka kuwa Grace Mapunda alifariki dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 2, 2024 katika hospitali ya Mwananyamala alipokuwa akipatiwa matibabu.

Grace enzi za uhai wake alionekana kwenye nyingi kama vile Mwaka wa Hasara, House of Death, Chungu ya Nafsi, Back to Life na nyingine nyingi. Wengi walimpenda kutokana na umahiri wake wa kuvaa uhusika.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags