Timu ya wanasheria wa Sean “Diddy” Combs, imeomba kesi inayomkabili rapa huyo kufutwa au kusitishwa kutokana na mapungufu katika ushahidi uliotolewa na baadhi ya watu akiwemo Cassie na rafiki yake Bryana Bongolan.
Inaelezwa kuwa ombi hilo jipya likiwa ni la pili kufikishwa mahakamani hapo limeonesha kuwepo kwa makosa kutoka serikalini kupeleka ushahidi ambao sio wa kweli kuhusu madai ya Diddy ambapo ombi hilo lilieleza kuwa rafiki wa Cassie, Bryana Bongolan alitoa taarifa za uongo kuhusiana na kukandamizwa kwenye kibaraza cha ghorofa tukio lililotokea Septemba 2016.
Barua hiyo iliendelea kueleza kuwa ushahidi kutoka kwa Ventura, mwenye umri wa miaka 38 kuhusiana na tukio la Bongolan haukustahiki kuwa kweli, kwani rekodi za meseji zinaonesha Ventura alipata taarifa juu ya tukio hilo baada ya kutokea.
Hata hivyo wakati wa uwasilishwaji wa picha za majeraha aliyoyapata Bongolan wakati wa tukio la ghorofa picha zilichukuliwa Septemba 26, 2016, huko Los Angeles lakini timu ya utetezi ya Diddy ilieleza ushahidi huo ni wa uongo kwani Septemba 24 hadi 29 mwaka huo, rapa huyo alikuwepo New York City.
Ikumbukwe timu ya utetezi ya Diddy ilianza kuomba kufutwa au kusitishwa kwa kesi tangu mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, baada ya mawakili wa mashtaka kumuuliza mpelelezi wa masuala ya moto wa Los Angeles, Lance Jimenez, kama ushahidi wa vidole na miguu katika tukio la bomu kwenye gari la Kid Cudi ulikuwa umeharibiwa ambapo Hakimu Arun Subramanian alikatisha swali hilo akieleza kuwa linaweza kuleta madhara makubwa kwenye kesi.
Hata hivyo, mawakili wa Diddy walisema endapo rapa huyo angehusika katika tukio hilo basi isingemlazimu kwenda mwenyewe bali angemlipa mtu ili kutekeleza hilo.
Mbali na hilo, Juni 6, 2025, katika Mahakama ya Shirikisho ya Manhattan, shahidi mwingine alipanda kizimbani aliyejitambulisha kwa jina bandia ‘Jane’ alieleza kuwa yeye na Diddy walikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kuanzia mwaka 2021 hadi alipokamatwa mwaka 2024.
Akitokwa na machozi wakati yupo kizimbani akitoa ushahidi, ameeleza kuwa Diddy alimlazimisha kushiriki kufanya matukio ya kingono yaliyojaa matumizi ya dawa za kulevya na wanaume waliolipwa.
Aidha aliendelea kwa kueleza kuwa rapa huyo alimlazimisha kufanya vitendo hivyo wakati wa hedhi, licha ya kujaribu kujiondoa kwenye matukio hayo kwa kutuma uthibitisho wa pads zenye damu lakini Diddy alikasirika huku akimuita muongo kupitia ujumbe wa sauti uliosikilizwa mahakamani.
Aliendelea kueleza kuwa alimwambia anywe shampeni ili kuendelea na matukio hayo ambayo yanachukua zaidi ya saa 30 huku tukio la mwisho likifanyika Agosti 2024, kabla ya kukamatwa kwa Combs.
Maelezo yake kuhusu matukio hayo, ambayo amesema Combs aliyaita "usiku wa hoteli," yanafanana sana na yale yanayoitwa "freak offs" yaliyotajwa na mpenzi wa zamani wa Diddy, Casandra "Cassie" Ventura.
Wanawake wote wawili walitoa ushahidi kwamba walilazimishwa kushiriki katika matukio hayo bila hiari yao, madai ambayo mawakili wa Combs wameyakanusha.
Utakumbuka Sean "Diddy" Combs alikamatwa Septemba 16, 2024 katika Hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan huko Brooklyn. Kesi yake ilianza kuzikilizwa Mei 5, 2025 huku mashahidi zaidi ya 15 wakitoa ushahidi akiwemo Kid Cudi, Mia, Cassie Ventura, mama mzazi wa Cassie, Bryana Bongolan na wengineo.

Leave a Reply