Zuchu anastahili saluti ya Dulla Makabila

Zuchu anastahili saluti ya Dulla Makabila

"Zuchu hata asingekuwa msanii wa Bongo Fleva angetokea tu mitaa ya pale kama msanii wa Singeli na bado angekuwa staa, anajua sana kuimba Singeli."

Hii ni kauli aliyoitoa hivi karibuni mfalme wa muziki wa Singeli nchini, Dulla Makabila kufuatia pafomansi nzuri aliyoifanya msanii wa Bongo Fleva, Zuchu baada ya kuachia ngoma kadhaa ambazo zipo katika mahadhi ya Singeli.

Zuchu amekuwa na muendelezo mzuri katika kutoa ngoma kali za Singeli akiwabamba mashabiki wengi kutokana na uwezo wake mkubwa katika kufanya muziki huo.

Kwa mara ya kwnza aliachia kazi ya Singeli kupitia wimbo wake wa 'Nyumba Ndogo' uliotoka (2021) ambapo alikuwa na mwaka mmoja na miezi mitatu tangu atambulishwe kama msanii rasmi kwenye lebo ya muziki inayomsimamia yeye na kazi zake, Wasafi.

Ukiachilia mbali wimbo huo kuwa mkali na kukubalika kwenye masikio ya mashabiki wengi kutokana na utunzi wake ambao upo ndani ya maudhui husika pia, ulimpa nafasi ya kuonesha uwezo wake wa ziada katika kufanya aina nyingine ya muziki, na sasa video ya wimbo huo imetazamwa zaidi ya mara milioni 41 kwenye mtandao wa Youtube.

Desemba 20, 2024 wakati anaachia albamu yake ya kwanza ya Peace and Money yenye nyimbo 13, ilishindwa kukamilika mpaka alipopata ngoma ya Singeli ya 'Hujanizidi' akiwa na D Voice ikiwa moja ya nyimbo zilizofanya vizuri katika albamu hiyo video yake ikifikisha kutazamwa zaidi ya mara milioni 6.6 ikiwa na miezi minne tangu kuachiwa kwake.

Zuchu amevuka kutoka kujipambania mwenyewe na kuanza kusimamisha hata wasanii wengine ambao jamii ilikuwa haijawapatia sikio na kuwatilia manani.

Aprili 26, aliingia kwenye historia ya maisha ya msanii mchanga wa Singeli, Dogo Paten baada ya kumbariki 'verse' kwenye wimbo wake wa Afande na kupanda naye kupafomu kwenye jukwaa la Samia Music Festival.

Zuchu kamtengenezea nafasi Paten kupitia wimbo wa Afande ambao umemtambulisha vema msanii huyo mchanga kwenye kiwanda cha muziki na mpaka sasa anapiga shoo kila kukicha kutokana na tagi ubavu alilopewa.

Mei 31, 2025, Zuchu alishirikishwa na msanii mwenzake kutokea lebo moja ya Wasafi, D Voice kupitia wimbo wa Singeli unaoenda kama Baby Mpya ambao umepokelewa kwa ukubwa audio yake ikifanikiwa kuingia kwenye trend ya muziki Youtube na kushika namba saba ikiwa na siku tatu tangu kutoka kwake.

Ndani ya miezi sita ya mwaka 2025, Zuchu amefanikiwa kushiriki nyimbo tatu za Singeli ambazo ni Hujanizidi, Afande, Baby Mpya.

Kwa muendelezo huo, mfalme wa muziki huo wa Singeli, Dulla Makabila alikuwa sahihi kuukubali uwezo wa Zuchu.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags