Wamepata familia ndani ya Bongofleva

Wamepata familia ndani ya Bongofleva

Peter Akaro

Mashabiki wanawaona kama wanamuziki waliopendana kisha wakafanya muziki, lakini kuna watu wanawatazama kama Baba na Mama wameamua kufanya muziki pamoja.

Hilo ni mara chache sana linatokea kutokana na mtindo wa maisha wa wasanii wengi. Hata hivyo kwenye Bongofleva kuna wasanii walikuwa wapenzi na pengine hadi sasa wapo pamoja, walifanya muziki wote na wakati huu wanatazamwa kama Baba na Mama. Hawa ni miongoni mwao;

Nahreel na Aika

Kundi hili liliundwa mwaka 2013 mara baada ya kuvunjika kwa kundi la Pah One, hata hivyo Nahreeh na Aika walikuwa wameanza muziki toka mwaka 2008 wakati wanasoma India (Punjab College) ambapo mapenzi yao yalianzia pia.

Mwaka 2014 Nahreel alifungua studio yake 'The Industry' baada ya kufanya kazi kwenye studio kadhaa kama Kawa Records chini ya G-Solo na Switch Records yake Quick Rocka.

Navy Kenzo ambao wameachia ngoma kali kama Kamatia Chini, Game, Fella, Katika, Why Now, Bajaj, Morning, Feel Good, Magical na nyinginezo. Tayari amejaliwa watoto wawili wa kiume, Gold na Jamaica.

Hadi sasa Nahreel na Aika wamefanikiwa kutoa albamu mbili, Above Inna Minute (AIM) iliyotoka Desemba 2016 ikiwa na nyimbo 11, pia kuna Story Of The African Mob iliyotoka Septemba, 2020 ikiwa na nyimbo 12.

Ruby na Kusah

Inafahamika kuwa Ruby ni mwimbaji mzuri wa studio na jukwaani, huku Kusah akiwa ni ni mwandishi mzuri wa nyimbo na ameshawaandikia wasanii kadhaa Bongo na nyimbo zao kufanya vizuri.

Hivyo kukutana kwao katika mahusiano ulikuwa ni mwanzo mwingine wa kuinuana kimuziki. Kusah ameandika wimbo wa Ruby uitwao Ntade ambao ulifanya vizuri sana na kumrudisha katika muziki baada ya ukimya.

Kwa kipindi walichokuwa wote walifanikiwa kutoa nyimbo tatu ambao ni Kelele,Chelewa na Nandondosha. Baada ya nyimbo hizo ukawa mwisho wa penzi lao wakiwa tayari wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kike,

Inaelezwa pia ugomvi wao hadi kufikia hatua ya kuachana ulianzia studio kwa kile kinachodaiwa ni mmoja wapo kuonyesha dharau kwa mwenzake.

Izzo Bizness na Abela Music (The Amazing)

Rapa Izzo Bizness na Abela Music waliunda kundi lijulikanalo kama The Amazing katikati ya mwaka 2016, Abela ni muimbaji aliyekuwa na makazi yake nchini Marekani mwenye asili ya Bukoba, Tanzania.

Mara baada ya kuunda kundi wimbo wao wa kwanza kuutoa unaitwa Dangerous Boy ambao ulitayarishwa na prodyuza Dupy wa Uprise Music huku video ikiongozwa na kampuni ya Focus Films chini ya Director, Nick Dizzo. Baada ya hapo waliweza kutoa nyimbo nyingine zilizofanya vizuri kama Umeniweza, Tumeoana na Rafiki.

Kipindi wakifanya kazi hizo walikuwa wakitupilia mbali tetesi za kuwa na mahusiano ya kimapenzi, hata hivyo mara baada ya Abela kujifungua watoto mapacha Aprili, 2018 akiwa Marekani ndipo ukapatikana uthibitisho kuwa wawili hao walikuwa na mahusiano ya kimapenzi.

Si hao tu, wapo pia Nandy na Billnass ambao walifunga ndoa mwaka 2022 na wamebarikiwa kupata mtoto mmoja aitwaye Naya

Ikumbukwe Billnass ameshiriki kuandika wimbo wa Nandy, Dah! (2024), na kwa ujumla wawili hao wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo ni Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags