Kama masihara, Dogo Rema huyoo anga za Bongo Fleva!

Kama masihara, Dogo Rema huyoo anga za Bongo Fleva!

Ni takribani miezi kadhaa tangu mtengenezaji maudhui mtandaoni na mfanyabiashara Dotto Magari kumtambulisha msanii wake, Dogo Rema ambaye amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii huku akifanyiwa masihara kutokana na aina ya uimbaji wake.

Licha ya baadhi ya watu kumbeza lakini kadri muda unavyozidi kwenda inaonesha wazi, Dogo Rema anazidi kupenya kwenye masikio ya wapenzi wa muziki. Huku wengi wakikiri mtandaoni kuyakumbuka mashairi ya nyimbo zake ambazo zimekuwa zikifanyiwa utani zaidi hasa wa ‘My everything’ maarufu kwa jina la ‘Tunedo’.

Msanii huyo amethibitisha kuwa hakuingia kwenye muziki kwa bahati mbaya kwa kuachia EP yake ya kwanza ‘Mtu Sie Nyau’ yenye nyimbo 3. Kupitia Ep hiyo imemwezesha Dogo Rema kuingia kwenye nyimbo 30 zinazofanya vizuri kwenye mtandao wa YouTube Tanzania.

Kupitia Ep amewagalagaza mastaa ambao wameachia ngoma hivi karibuni ikiwamo Best Couple ya Harmonize na Down ya kwake Diamond Platnumz.

Nyimbo zake zote tatu zimefanikiwa kuingia katika chati hizo ambapo wimbo wa Weekend ukishika nafasi ya 15, Inatokeaga ikiwa namba 16 na See You ikishika nafasi ya 21.

Maoni mseto ya wadau

Akizungumza na Mwananchi, Nadi kutokea mtaa wa Tabata jijini Dar es Salaam, amesema Dogo Rema kwenye muziki bado ila mashabiki wanafurahia vituko vyake.

"Dogo Rema kwenye muziki bado na sio kwamba hajui kidogo, yaani hajui kabisa. Cha msingi sisi mashabiki tunaangalia vituko vyake sio kwamba uimbaji hapana. Ni vituko na nguo zake ambazo anatuvalia kwa hiyo tunafurahia kuangalia ile minguo yake ila hatufurahii muziki wake," amesema Nadi.

Amesema mashabiki wamempokea na kumwonesha sapoti kwa sababu amekuja kitofauti hususani uvaaji wake wa kipekee ukilinganisha na wasanii wengine.

"Mashabiki wamempokea kwa sababu amekuja na njia ya kitofauti hakuna msanii amewahi kuvaa minguo kama ile maana yake amekuja na mtindo wake wa vituko, mimi hata nikikutana naye nashangaa zile nguo sio kuimba kwake," amesema Nadi.

Kwa upande wake Fami Innocent, ambaye ni mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam amesema Dogo Rema anajitahidi na anafanya vizuri kikubwa apambane bila kusikiliza maneno ya mashabiki wanaomponda.

"Dogo Rema anajitahidi na anafanya vizuri, kikubwa aongeze juhudi apambane na asisikilize mashabiki wanaongea nini. Mwingine anaongea anakuponda kikubwa ni asimamie mambo yake tu.

“Muziki ulivyo unaweza kukuta msanii anaonekana anapuyanga lakini ndiyo anatembea hivyo, mimi naona ana kitu. Japo meneja wake Dotto Magari muongeaji sana lakini Dogo Rema tayari ameshakubali matokeo," amesema Fami.

Naye mwanadada Naomi Kane mkazi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam amesema Dogo Rema kipaji chake cha muziki ni kidogo lakini anatakiwa apambane bila kukata tamaa kwani wasanii wengi wakubwa walianza kama yeye.

"Dogo Rema kweli kipaji chake ni kidogo lakini anatakiwa apambane wengi wametokea huko huko wamejitafuta mpaka sasa wamekuwa wasanii wakubwa kwa hiyo asikatishwe tamaa na maneno ya watu. Anatakiwa asimamie misingi yake kama anataka kutoka zaidi na afanye muziki wake vizuri Mungu atamjalia na watu watamwelewa," amesema Naomi Kane.

Amesema namna ambavyo meneja wa msanii huyo, Dotto Magari anavyofanya naye maudhui ya mtandaoni sio kumwaibisha bali anamsaidia ili mashabiki waendelee kumfuatilia zaidi.

"Hapana hamwaibishi pia hiyo ni moja kati ya maudhui na njia yao huwezi jua inamwongezea watazamaji na watu kumfuatilia zaidi kwenye muziki wake na mitandao ya kijamii," amesema Naomi Kane.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags