Mama wa mwanamuziki Sean Kingston, Bi Janice Turner (63) amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia pamoja na mwanae Kingston katika kesi ya madai ya kufanya udanganyifu katika biashara yenye thamani zaidi ya dola milioni 1 za Kimarekani.
Kabla ya kuhukumiwa, Turner alimwambia hakimu, "Samahani. Nia yangu ilikuwa kumsaidia mwanangu katika tasnia hii ngumu. Walimtumia na kumdhulumu. Ninaomba huruma kwa ajili yangu na mwanangu."
Utakumbuka, Sean Kingston na mama yake Janice Turner wanahukumiwa kutokana na madai ya kufanya udanganyifu wa biashara yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 1 za Kimarekani, ambapo kesi hiyo inahusisha vito vya thamani, magari ya kifahari, na bidhaa nyingine zenye gharama kubwa.
Mashtaka hayo yanahusisha udanganyifu kwa muuzaji wa magari yenye thamani ya dola 160,000. Pia kudanganya wauzaji wa vito vya thamani kwa bidhaa zenye thamani ya dola 480,000, na vitu vingine.
Turner na Kingston walikamatwa Mei 23, 2024. Mwimbaji huyo aliwekwa mahabusu katika kituo cha mafunzo cha Jeshi la Marekani huko California, Fort Irwin huku Turner alikamatwa katika jumba la South Florida ambalo Kingston alikuwa amekodisha. Wakati wa kukamatwa kwake, Kingston alikuwa akitumikia kifungo cha miaka miwili kwa kusafirisha mali ya wizi.
Hati za kukamatwa zilielezea hasara waliyosababisha Kingstone na mama yake kuanzia Oktoba 2023 hadi Machi 2024, ikijumuisha karibu dola 500,000 za vito vya thamani, dola 200,000 kutoka Benki ya Marekani, dola 160,000 kutoka kwa mfanya biashara wa SUV, zaidi ya dola 100,000 kutoka First Republic Bank, na dola 86,000 kutoka kwa mtengenezaji maalum wa kitanda.
Hii sio mara ya kwanza kwa Janice Turner kushitakiwa kwa makosa ya ulaghai, utakumbuka mwaka 2006 alikiri makosa ya ulaghai aliyoyafanya benki ambapo alitumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu gerezani kwa kuiba zaidi ya dola 160,000, kwa mujibu wa rekodi za mahakama.
Hata hivyo, Kingston ambaye hukumu yake itatolewa Agosti 28, 2025, alijipatia umaarufu mwaka 2007 baada ya kuachia wimbo wake wa 'Beautiful Girls' na baadaye akashirikiana na Justin Bieber kwenye wimbo wa 'Eenie Meenie'

Leave a Reply