Rapa Cash Out, ambaye jina lake halisi ni John-Michael Hakeem Gibson, amehukumiwa kifungo cha maisha jela pamoja na miaka mingine 70 siku ya Jumatatu baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya uhalifu wa mtandao (RICO) na usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono.
Siku ya Ijumaa, Cash alipatikana na hatia katika mahakama ya Atlanta. Kwa mujibu wa kituo cha WSB-TV cha Atlanta, amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la ubakaji pamoja na kifungo cha ziada cha miaka 70 kwa makosa ya RICO na mengineyo, ambapo kifungo hicho kitatekelezwa kwa pamoja.
Mbali na rapa huyo lakini pia Mama yake mzazi, Linda Smith, alihukumiwa kifungo cha miaka 30, na binamu yake, Tyrone Taylor, alihukumiwa kifungo cha maisha pamoja na miaka mingine 70.
Kesi hiyo, ambayo ilianza kusikilizwa miezi miwili iliyopita, ilihusu madai kwamba Cash Out, mama yake na binamu yake waliwalazimisha wanawake kufanya kazi za ngono kwa kipindi cha miaka saba.
“Hili limekuwa likiendelea kwa miaka saba,” alisema mwendesha mashtaka wa Kaunti ya Fulton, Earnelle Winfrey, mbele ya mahakama ya Atlanta siku ya Ijumaa. “Hii siyo ukahaba wa kawaida hii ni usafirishaji wa binadamu na biashara za kingono,”amesema
Cash alikabiliwa na mashtaka kwa mara ya kwanza mwezi Juni 2023. Timu yake ya wanasheria ilidai kuwa waathirika walilazimishwa kutoa ushahidi. Katika hoja za mwisho, walisisitiza kuwa wanawake waliohusishwa hawakulazimishwa bali walishiriki vitendo hivyo kwa hiari.
Hata hivyo mama yake alidai kuwa hakuwa na ufahamu wowote kuhusu biashara hiyo ya usafirishaji wa binadamu, lakini waendesha mashtaka waliwasilisha risiti za malipo zilizomhusisha moja kwa moja na makosa hayo. Ushahidi huo ulijumuisha pia nyumba ya kupangisha ‘Nyumba ya Mateso’ ambapo baadhi ya waathirika walidaiwa kuwa ndio ilikuwa sehemu ya kufanyia vitendo hivyo.
Rapa huyo alianza kupata mafanikio mwanzoni mwa mwaka 2010, kupitia wimbo wake wa kwanza “Cashin’ Out,” ambao uliongoza chati ya Billboard Rap Airplay. Alipata umaarufu tena na wimbo wa “She Twerkin” miaka miwili baadaye, alifanikiwa kutoa albamu yake pekee, ya “Let’s Get It.”

Leave a Reply