Mzalishaji na mwongozaji wa tamthilia ya ‘Jua Kali’, Leah Mwendamseka 'Lamata' ameelezea alivyopokea taarifa za kifo cha muigizaji wa tamthilia hiyo, Raidanus Vitalis ‘Kitundu’ aliyefariki dunia jana Juni 24, 2025.
Akizungumza na Mwananchi, Lamata amesema taarifa za msiba huo alipokea jioni ya Juni 24, 2025, wakati akiwa safarini akitokea Iringa kwenda Dar Es Salaam.
“Taarifa nilipata jana nilikuwa natokea Iringa narudi Dar ilikuwa jioni, alikuwa anaumwa kwahiyo siwezi kuelezea zaidi mwanafamilia ndio anatakiwa kuongea zaidi, mimi ni kama bosi wake, ilikuwa ni ugonjwa alitetereka kiafya,” amesema Lamata.
Kuhusu kuumwa kwake, Lamata amesema Kitundu alianza kuumwa mwaka jana na kupelekea kutoshiriki vizuri kwenye tamthilia ya Jua Kali.
“Ni kuanzia mwaka jana, aliumwa kidogo akakaa sawa akarudi kuigiza lakini akaumwa tena, basi ikawa hivyo,” amesema Lamata.
Aidha ameweka wazi kuwa taarifa zaidi kuhusu mazishi ya mwigizaji huyo zitatolewa baadae, kwasasa bado wanaendelea kufuatilia utaratibu wa msiba huo.
"Tutawajulisha baadae, ndio tupo hapa tunafanya utaratibu" amesema.
Naye mchekeshaji na mwigizaji Jol Master, ameelezea namna alivyopokea taarifa za msiba huo.
“Nilipokea kwa majonzi sana kwa sababu ni mwigizaji mwenzetu, tumefanyakazi kwenye tamthilia moja, kwahiyo ni machungu, ni taarifa ambayo imeniumiza sio tu mimi hata wadau na mashabiki kwahiyo tupewe pole sisi wasanii na Mwenyezi Mungu ailaze roho mahala pema sana,” amesema Jol Master.
Amesema hakuwa na ukaribu na marehemu Kitundu, lakini alishitushwa baada ya kuona taarifa za kifo chake iliyotolewa na Lamata kupitia kundi la WhatsApp la wasanii wa Jua Kali.
“Nisiwe muongo, marehemu sikuwa na mazoea naye sana au tulikuwa tunakutana mara kwa mara, hata kutokuonekana kwake muda mrefu sikuwahi kujua kama anaugua, hata taarifa yake ilivyotumwa kwenye grupu ilitumwa picha yake, mara ya kwanza sikujua kama kafariki, lakini sasa nilivyosoma ujumbe wa Lamatta ndio nikajua kafariki," amesema Jol Master.
Hata hivyo, mastaa wengine wameelezea hisia zao kupitia mitandao ya kijamii juu ya taarifa hiyo ya msiba wa Kitundu, akiwemo msanii wa Bongo Fleva Chino Kidd ambae amendika "Furaha yao kutuona tunakufa kwa dharau, ila one day kila kitu kitaisha, na sisi tutaheshimika, na familia zetu zitafurahia na kutajirika kutokana na talent zetu. R.I.P mwanangu KITUNDU 😭😭😭🙏 Japokuwa imeniuma sana kichaa wangu daaah." ameandika Chino.
Naye mwigizaji na Mwanamuziki, Quick Rocka ameweka picha ya marehemu Kitundu na kuandika:
"Dogo lao umeenda mapema sana 🕊️ Pole kwa familia, familia ya Juakali, marafiki na mashabiki wa Kitundu. R.I.P Kitundu." ameandika
Kwa upande wa , Sophy Juakali aliandika "Kitundu mdogo wangu umeniuma pumzika kwa amani 😭😭😭😭😭" Kajala Masanja ameandika "Daaaah tumepoteza mtoto wetu 😭😭😭😭😭😭😔💔" Wolper Stylish nae ameandika "Nimeumia sana", lakini pia mashabiki pamoja na wadau wengine wa burudani wamemiminika kwenye chapisho la taarifa hiyo ya msiba wakionesha kusikishwa.
Enzi za uhai wake, Kitundu aliigiza kwenye tamthilia hiyo kama kijana mwenye kipaji cha kucheza muziki anayetokea kwenye familia ya kimasikini. Kisha baadaye anapata nafasi ya kutoboa kimaisha lakini anashindwa kuitumia vizuri na kujikuta akirudi kwenye maisha ya kimasikini.
Mwananchi inaendelea kufanya juhudi za kuwatafuta watu wa karibu wa marehemu kuzungumzia kwa kina kuhusu taratibu za msiba huo zinavyofanyika. Apumzike kwa amani Kitundu.

Leave a Reply