Inaelezwa kuwa hukumu ya Sean 'Diddy' Combs itatolewa Oktoba 3,2025 kwa makosa mawili likiwemo la kuhusika na biashara ya ukahaba, hatua hiyo imefikiwa baada ya wanasheria wake na waendesha mashtaka kufikia makubaliano.
Mawakili wa rapa huyo waliwasilisha rasmi pendekezo la tarehe hiyo ya hukumu kwa Jaji Arun Subramanian, wakieleza kuwa waendesha mashtaka na maofisa wa uangalizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kusini mwa New York walikubaliana na ratiba hiyo.
Kulingana na hati ya makubaliano iliyotiwa saini na jaji Subramanian jana Julai 8,2025, hati ya utetezi kuhusu hukumu hiyo itawasilishwa Septemba 19,2025 na upande wa mashtaka utaweka hoja zake wiki moja baadaye.
Uamuzi huo ulifanywa na mawakili wa pande zote mbili ambapo walishiriki kwenye mkutano mfupi kwa njia ya simu Jumanne alasiri, bila uwepo wa Combs wala Jaji Subramanian.
Combs, ambaye alikabiliwa na kesi iliyodumu kwa takriban miezi miwili, alipatikana na hatia ya makosa mawili ya kusafirisha watu kwa ajili ya kujiingiza kwenye ukahaba, lakini alifutiwa mashtaka ya usafirishaji wa binadamu na makosa ya kupanga njama za kihalifu.
Ikumbukwe baada ya uamuzi kufanyika mawakili wa Combs waliomba aachiliwe kwa dhamana ya dola milioni 1, lakini ombi hilo lilikataliwa na jaji Subramanian, baada ya serikali pamoja na mpenzi wake wa zamani, Casandra “Cassie” Ventura, kuwasilisha hoja kuwa Combs abaki rumande hadi siku ya hukumu, wakidai kuwa anaweza kutoroka na pia ni tishio kwa waliotoa ushahidi dhidi yake.
Aidha kwa mujibu wa vyanzo vya karibu vinaeleza kuwa Serikali inataka Combs ahukumiwe kifungo cha kati ya miezi 51 hadi 63 jela, huku upande wa utetezi unapendekeza kifungo kifupi cha kati ya miezi 21 hadi 27.
Combs ataendelea kuzuiliwa katika gereza la Metropolitan lilichopo Brooklyn hadi siku ya hukumu, ambapo kuna uwezekano atapewa punguzo la muda aliokaa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Sean "Diddy" Combs alikamatwa Septemba 16, 2024 katika hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan. Kesi yake ilianza kusikilizwa Mei 5,2025 huku watu mbalimbali wakitoa ushahidi akiwemo mpenzi wake wa muda mrefu Cassie Ventura, Jane, Mia, Kid Cudi, Bongolani, mama mzazi wa Cassie na wengineo.

Leave a Reply