Ukiachilia mbali msanii kuwa na uandishi mzuri, Sauti, Floo, Midondoko na Melodi kali za kuvutia pia anahitaji tiketi ya kukubalika na mashabiki iliaweze kufanikiwa kwenda mbali zaidi kimuziki.
Wasanii wa Bongo Fleva ambao wamedumu kwenye gemu kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo, wanastahili heshima kwani mashabiki wa muziki huo wanatoa sapoti kwa kila msanii anayefanya vizuri hivyo ni ngumu kubaki kumsikiliza msanii mmoja kwa kipindi cha muda mrefu.
Ukitaka kuamini hilo fuatilia kazi nyingi ambazo zimeachiwa hivi karibuni kwa mwaka huu 2025, kutoka kwa wasanii wakubwa na wadogo kama zimekaa trendi, kwenye majukwaa ya muziki sio zaidi ya wiki tatu lazima zishushwe na nyimbo nyingine tofauti kutoka kwa msanii mwingine.
Wadau wengi wa muziki huita nyimbo hizo zinazochuja ndani ya muda mfupi 'Babogum Music', yaani Big G ambayo hutafunwa ndani ya muda mfupi kisha huisha utamu wake.
Tumeshuhudia wasanii wengi wakijitahidi kuachia kazi lakini bado zinachuja sio tu kwenye chati za muziki pekee bali hata kwa mashabiki, ni ngumu kukuta shabiki anasikiliza nyimbo zilizotoka miaka miwili iliyopita lakini utakuta anasikiliza ngoma mpya ambayo inatrendi kwa muda huo.
Mfano hivi karibuni zimeachiwa projekti kali kutoka kwa wasanii lakini zimepotea masikioni mwa mashabiki na kwenye chati za muziki, mfano wa kazi hizo ni pamoja na Ep ya mkali wa Bongo Fleva, Juma Jux ' A Day to Remember' iliyotoka Mei 23, 2025, ikiwa na mikwaju saba ya maana kabisa, lakini ukiachana na ngoma ya God Design, na Si Mimi ambazo zilitangulia kutoka kabla ya Ep hiyo kuachiwa rasmi hakuna wimbo mwingine uliopenya zaidi licha ya kuwa na ngoma kali kama Ololo, Shayla, You, Celebration, Ex wa Nani.
Pia, msanii wa Bongo Fleva, Jay mwenye Melody zake aliachia Albamu yake ya 'Addiction' Mei 9, 2025, ikiwa na nyimbo 12, ambapo kati ya nyimbo hizo zipo zilizopokelewa kwa ukubwa ndani ya muda mfupi kama Tila Lila, Jirani, Mara ya kwanza lakini projekti hiyo imekuja kuzimwa na kama mshumaa na harusi ya Jux iliyoambatana na Ep yake ya 'A Day to Remember.'
Msanii Barnaba aliachia ngoma yake ya Salama akiwa na Diamond Platnumz iliyotoka Mei 16, 2025, ngoma ambayo ilipokelewa vizuri na mashabiki baada ya kuachiwa kwa video yake Juni 31, 2025, lakini ngoma hiyo pia ilikuja kushushwa na Double Release kutoka kwa Diamond Platnumz ambazo ni Katam akiwa na Bien, na Babu akiwa na Master Piece Yvk.
Lakini pia, kama umechunguza kwa sasa Ep ya Mbosso imeweza kupenya na kufanya vizuri zaidi mitandaoni na mtaani ikizishusha projekti ambazo zimetoka ndani ya muda mfupi kabla yake.
Nyimbo zinazopotea kwenye chati na masikioni mwa mashabiki ndani ya muda mfupi zote zimetoka mwaka huu ndani ya mwezi mmoja je, vipi kuhusu zile ambazo zimetoka miaka miwili hadi mitatu nyuma.
Utaratibu huo wa Kuhiti na kutrendi haraka kisha wapishe wenzako unawafeva wasanii wenye bajeti kubwa ya kuweza kuachia kazi mara kwa mara na ndio maana kila siku wanatrendi na kuhiti walewale, msanii anayejitafuta akifanikiwa kuachia ngoma ikaenda mjini na kupokelewa kwa ukubwa mafanikio hayo huambatana na msongo wa mawazo namna gani anaweza kufanya jambo likawa kubwa kama alivyo weza mwanzo, na ndiomaana utasikia kila siku "Dogo Paten mbona hatumuoni kuachia kazi baada ya Afande"

Leave a Reply