Wawili hao walionekana kwa mara ya kwanza Julai 19, 2024 kwenye moja ya kumbi za starehe zilizopo jijini Dar es Salaam huku uhusiano huo ukiwekwa wazi katika mitandao ya kijamii Agosti mwaka huohuo baada ya Jux kupokelewa kwa shangwe ukweni Nigeria.
Ndoa hiyo iliyofanyika nyumbani kwa Jux, ilihudhuriwa na watu wachache wakiwemo ndugu wa karibu pamoja na wasanii kama vile Diamond Platnumz, Zuchu, S2kizzy, Abba, Ommy Dimpoz na wengine.

Priscilla ni nani?
Jina kamili anaitwa Priscilla Ajoke Ojo, alizaliwa Machi 13, 2001 Jimbo la Lagos, Nigeria, asili yake ikiwa ni kutoka jimbo la Ogun, ni mtoto wa mwigizaji mkongwe Nollywood Iyabo Ojo, ambaye ameshiriki katika filamu zaidi ya 150 na kutoa zake binafsi 14 huku baba yake akifahamika kwa jina la Ademidun Ojo.
Priscilla alimaliza masomo yake ya sekondari mwaka 2017 katika shule binafsi mashuhuri kwenye Kisiwa cha Lagos na kupata nafasi ya kujiunga katika Chuo Kikuu cha Babcock, kilichopo Ilishan-Remo, Nigeria, ambako alisomea Masuala ya Vyombo vya Habari na Sanaa ya Maigizo ‘Media and Theater Arts’ na alihitimu mwaka 2021.
Mrembo huyo alianza kujihusisha na uigizaji akiwa na umri wa miaka 14, filamu yake ya kwanza ikiwa ni ‘Beyond Disability’ ambayo ilimletea umaarufu na kumfanya apate uteuzi katika tuzo za ‘Best of Nollywood’ katika kipengele cha Mwigizaji Bora Mdogo.
Amewahi kuonekana kwenye filamu nyingine mbalimbali zikiwemo Silence (2016), Victims (2017), Blackmail (2018), Undercover Lover (2019) na nyinginezo ambazo ameshiriki na rafiki yake mkubwa wa kiume ambaye pia alikuwepo kwenye sherehe ya ndoa yake aitwaye Enioluwa Adeoluwa.

Mbali na uigizaji, Priscilla ni mwanamitindo na mshawishi mkubwa katika mitandao ya kijamii hasa Instagram, kutokana na umaarufu wake amekuwa akisaini madili ya maokoto kupitia kampuni mbalimbali, lakini pia ni mmiliki wa duka la mtandaoni la mavazi linaloitwa Priscy Closet. aidha kupitia ukurasa wake wa instagram ameweka jina lingine alililopewa baada ya kubadilisha dini ambapo kwasasa anaitwa Hadiza Mkambala.
Leave a Reply