Kampuni inayohusika na kuonesha filamu ya ‘Squid Game’, Netflix imethibitisha hitimisho ‘Final’ ya filamu hiyo kutoka wiki hii, msimu wa tatu wa Squid Game unatarajiwa kuachiwa rasmi Juni 27,2025.
Kupitia ukurasa wao wa Instagram, Netflix wamethibitisha taarifa hiyo kwa kuandika “Mchezo karibu unafikia mwisho. Tamati ya Squid Game itaonyeshwa Juni 27, ni kwenye Netflix pekee,”
Aidha taarifa hiyo imeibua mijadala katika mitandao ya kijamii ambapo mashabiki mbalimbali wametoa maoni yao kwa kuandika “Naogopa mwisho utakavyokuwa, najua kutakuwa na maumivu,”, “Mchezo wa msimu huu ni wa kichaa! ‘Squid Game angani’? Hii ni balaa,” ,” Michezo ya msimu huu ni ya kichaa! ‘Squid Game angani’? Hii ni balaa,” huku mwingine akiandika “Season ya pili ilinibo, lakini natumaini tamati itakuwa kali,”.
Utakumbuka msimu wa kwanza wa Squid Game ambao uliachiwa rasmi Septemba 17, 2021 uliweka rekodi kushinda tuzo sita za Primetime Emmy, ikiwemo tuzo ya kihistoria kwa mkurugenzi Hwang Dong-hyuk, ambaye alishinda tuzo ya Outstanding Directing kwa Drama Series. Waigizaji Lee Jung-jae na Lee You-mi pia walishinda tuzo kwa ufanisi wao.
Vilevile Netflix iliripoti kuwa ulikuwa ni mfululizo wake maarufu zaidi duniani kwa kipindi hicho, ikifikisha zaidi ya watu milioni 142 wakifungua akaunti kuangalia filamu hiyo pamoja na kupata watazamaji bilioni 2.2 katika wiki yake ya kwanza.
Aidha msimu wa pili wa Squid Game uliachiwa rasmi Desemba 26, 2024 ukinogeshwa na mastaa kama Lee Jung-jae, Lee Byung-hun, Wi Ha-jun, na Gong Yoo. Huku kukiwa na washiriki wapya kama Yim Si-wan, Kang Ha-neul, Park Gyu-young, Lee Jin-uk, Park Sung-hoon, Yang Dong-geun, Kang Ae-sim, Lee David, Choi Seung-hyun, Roh Jae-won, Jo Yu-ri, na Won Ji-an.
Filamu hiyo maarufu ya Kikorea iliripotiwa kuweka rekodi kwa kushika namba moja kwenye nchi zaidi ya 93 ikiwemo Marekani, Honduras, Kenya, Oman, Thailand na nyingine, pia ilifanikiwa kupata watazamaji milioni 68 ndani ya siku nne za kwanza. Rekodi ambayo hapo awali ilishikwa na filamu ya Wednesday, ikipata watazamaji milioni 50.1 katika wiki yake ya kwanza.
Msimu wa kwanza uliingiza zaidi ya dola milioni 900 kwa Netflix, huku ikigharimu takribani dola milioni 21.4 tu kutengenezwa, hata hivyo Squid Game (msimu 1 & 2) umekadiriwa kuingiza zaidi ya dola bilioni 1 kwa Netflix.

Leave a Reply