Mwili wa aliyekuwa mwigizaji wa filamu nchini, Raidanus Vitalis ‘Kitundu’ unatarajiwa kuzikwa kesho Alhamisi Juni 26, 2025, katika makaburi ya Wailes yaliyopo Temeke jijini Dar Es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, mwigizaji wa tamthilia Jua Kali, Abdul Razak anayecheza kama 'Davis' kwenye filamu hiyo, ameeleza ratiba ya mazishi ya Kitundu itaanza saa 4 asubuhi nyumbani kwao Vikindu mtaa wa Magomeni.
“Msiba upo nyumbani kwao Vikindu mtaa wa Magomeni, kuzika kesho tarehe 26, muda wa kuaga saa 4 asubuhi kwao Vikindu. kuzika ni saa 8 mchana makaburini Wailes Temeke karibu na Chang'ombe Polisi. Namba ya mawasiliano kufika pale nyumbani ni 0785975656," amesema Abdul.
Kitundu amefariki dunia jana Juni 24, 2025, ambapo taarifa za msiba huo zilitolewa kupitia ukurasa wa Instagram wa mzalishaji na mwongozaji wa tamthilia aliyokuwa akiigiza ya ‘Jua Kali’, Leah Mwendamseka 'Lamata.'
Enzi za uhai wake, Kitundu aliigiza kwenye tamthilia hiyo kama kijana mwenye kipaji cha kucheza muziki anayetokea kwenye familia ya kimasikini. Kisha baadaye anapata nafasi ya kutoboa kimaisha lakini anashindwa kuitumia vizuri na kujikuta akirudi kwenye maisha ya kimasikini.
Lamata alibainisha kuwa kabla ya Kitundu kufariki, alikuwa anaumwa tangu mwaka jana na kupelekea kutoshiriki vizuri kwenye tamthilia ya Jua Kali huku akishindwa kutaja kilichokuwa kinamsumbua zaidi.
Mwananchi inaendelea kufanya juhudi za kuwatafuta watu wa karibu wa marehemu kujua kilichokuwa kinamsumbua hadi kusababisha kifo chake. Apumzike kwa amani Kitundu.

Leave a Reply