Ndani Ya Boksi: Mbosso Kila Harusi Milioni 50

Ndani Ya Boksi: Mbosso Kila Harusi Milioni 50

Issa Matona. Mishangazi na midingi inamjua. Mwamba kutoka Visiwani. Alikuwa ni mwanamuziki wa taarabu. Lakini taarabu yake ilikuwa tofuati na hii ya kina Mzee Yusuf na wenzake. Yeye alikuwa wa pekee.

Upekee ulitokana na zile tungo zake. Alikuwa na kitu ndani yake, hata pale alipopoteza maisha. Kwa kugongwa na gari mitaa ya Upanga. Akielekea kwenye shoo pale Diamond Jubilee. Ilitafakarisha sana. Noma.

Tulio wengi hatukuumizwa na kifo tu, bali maisha yake. Inakuaje Matona Issa Matona, anatembea kwa miguu usiku kwenda kwenye kazi yake? Issa Matona huyu huyu, ambaye kafanya kila kitu kwenye taarabu? Iliumiza sana.

Harusi gani mitaa ya huku Pwani bila nyimbo zake? Shughuli gani mitaani bila ngoma za Muunguja huyu? Sasa kwanini aishi maisha yale? Ajali ya gari, sawa inawezekana. Lakini siyo ajali ya gari kwa kugongwa yeye na gari akiwa kwa miguu.

Pale nikashindilia msumari wa neno “Kipaji na maisha ya ovyo ni kulwa na doto.” Lakini msamiati huu unafanya kazi huku Vingunguti na Bonyokwa. Wenzetu kipaji na utajiri ni samaki na maji. Kwenye hili hakika dunia haina usawa, abadani.

Issa Matona ‘bigi nemu’ Afrika yote ya Ukanda wa Mashariki. Mpaka kesho nyimbo zake zinabariki harusi kitaani. Watu wanaimba nyimbo zake akiwa tayari ni mchanganyiko wa mwili na udongo. Fundi huyu wa maneno toka Unguja mwenye upwani pwani wake.

Wakati Matona akiwa hayupo nasi kwa mapenzi ya Mola. Ni Mola huyo huyo hajatuacha bure, ametupa tena Matona wa kizazi kipya. Inawezekana muziki wa Matona wa dunia ya sasa si sawa na muziki wa Matona wa kale. Ila ni walewale kwa mengi.

Namuongelea fundi wa muziki mtoto mdogo. Asiye na makuu wala fujo za kuumiza. Asiye na maneno mengi na mtulivu katika kazi yake. Mbosso ndo jina tunalotaka kuliongelea kwa hii leo hapa. Weka kila kitu pembeni, shikilia vyema gazeti lako. Nisome.

Tunamuongelea Mbosso Khan. Kama humpendi, basi demu au dadaako humwambii kitu kwa huyu kiunmbe. Anapendwa na madem, na siyo kwa uzinzi, bali kwa muziki wake bora. Jamaa ana kipande chake cha muziki kisichoingiliana na wengine.

Hafanani na mwanamuziki mwingine. Mbosso yupo kivyake vyake kuanzia uvaaji, uimbaji mpaka na utunzi wake. Kuna jambo moja, ambalo wengi wao hawaelewi. Msanii mkali mara nyingi hafananii na kazi anayofanya, ni kama Mbosso. Huwezi kumdhania.

Ukikutana naye ni ngumu kumuamini kuwa ni yeye. Yule anayewaimbisha kina majimama, mijishangazii na zile pisi za ‘jenzii’ kila kona. Huyo dogo ana ‘pawa’ ya muziki kuliko ‘pawa’ ya mwili. Wa Ya Moto Band, ni yule yule na huyu wa sasa. Hajabadilika.

Hanyanyui bega. Hafanyi mahojiano ya kijinga. Heshima yake kwa wadau haitofautiani na ile ya mabosi wake. ‘Bigi Bosi’ wake Diamond Platinumz, nilimuelewa aliporuhusu dogo asepe bila kulipa chochote. Heshima yake imemlipa Mbosso.

Heshima ndo inamfanya yule Queen Darleen ampende. Tena kwa upendo wa ‘agape’. Queen Darleen hajawahi kufeki kumhusudu huyu dogo. Na nimedokezwa na wapuuzi wa mjini, kwamba alichangia sana Mbosso asainishwe WCB Beibi.

Madogo wenye heshima sampuli hii ni wachache sana. Hata utazame katika familia yako, si ajabu hakuna mwenye tabia za Mbosso. Ukiwepo wewe pia. Siyo kwamba ana njaa ama maisha. Ndo tabia yake inayofanya ajishushe. Asijikweze ovyo.

Huyu ni Issa Matona mwingine. Ndo maana hata alipozingua na ile video yake. Alipoitwa Basata umma ulikuwa nyuma yake, kwa namna flani hivi. Iko hivi! Jamii inaweza kukuunga mkono kwa kukaa kimya kwenye tatizo lako. Ukiwa na makosa.

Na utulivu wako ndo unaofanya jamii iwe na wewe kwa shida na raha. Video ile angekuwa ni msanii mwingine, bila shaka kelele zingetawala. Ila Mbosso ikawa kimya kimya na ile kesi ikaisha kimya kimya. Na maisha yanaendelea kama kawa.

Kwa aina ya muziki wake. Namuona Issa Matona ndani yake. Na yeye pia muziki wake unachezwa sana katika shughuli za namna hii. Dogo soko lake lipo kwenye mioyo ya kikeni. Ogopa mtu aliyekamata mioyo ya watoto wa kike.
Ningekuwa meneja wa Mbosso, nisingehangaika na shoo za nje wala ndani. Ningejitafutia eneo la biashara yangu kwenye shughuli hizi za kijamii. Mbosso anaweza kulipwa milioni 50 kwa shoo moja ya harusi tu. Na ratiba yake ikawa full kila mwisho wa wiki.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags