Kila msanii wa muziki huwa na zawadi yake ya kipekee aliyobarikiwa katika uwezo na uwasilishaji wa kazi zake. Wapo wenye sauti nzuri,kupendwa na mashabiki, melodi kali na wengine utunzi uliotukuka.
Kwa mkali wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz amekuwa na uwezo mkubwa katika kuandika na kufanya aina tofauti tofauti za muziki kama alivyosema kwenye mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mei 21, 2025.
“Mimi uwezo wangu umetokana na kuandika. Yaani mimi kama mwanamuziki nikishika peni naweza nikakuandikia wimbo wowote. Iwe Bolingo, R&B, Kibao Kata, Hiphop, Amapiano na kila muziki najua niandike vipi,” alisema Diamond.
Unaweza kusema kauli hiyo haijakaa kwa ajili ya kujikweza kwani, Diamond rasmi aliachia wimbo wake wa kwanza 'Kamwambie' 2010 na kutambulika vizuri. Kisha baadaye kuachia nyingine kama 'Moyo Wangu', 'Kesho' na nyingine nyingi zilimuwezesha kupenya kwenye soko la Afrika Mashariki na kimataifa
Baada ya msanii huyo kupenya kwenye soko Afrika Mashariki alianza kunyemelea soko la Afrika Magharibi hususani nchini Nigeria ambapo muziki wao ulikuwa umepiga hatua. Diamond alifanikiwa kufanya Kolabo na wasanii kama Davido 'My Number One' (2014),Nana (2014) akimshirikisha Mr Flavour, Bum Bum (2014) akiwa na Iyanya mwaka huohuo alishirikishwa na kundi la Bracket kwenye ngoma yao 'Alive', 'Kidogo' ya 2016 akiwa na P'square, Fire 2017 akiwa na Tiwa Savage na nyingine nyingi.
Hata hivyo wakati muziki wa Afrobeat kutokea Nigeria ukishika kasi miaka mitano iliyopita, Diamond alifanikiwa kufanya muziki huo na wasanii wakali wa muda huo kama Teni kupitia ngoma ya Sound (2019), Gimmi (2021) ft Rema, (2020) RJ The Dj aliwakutanisha Diamond Platnumz na Ceeza Milli kwenye ngoma ya Rotate, mwaka 2020 pia Krizbeatz aliwashirikisha Diamond na Ceeboi kwenye ngoma ya 'Abi'.
Diamond pia alipenya kwenye soko la muziki wa Afrika Kusini tangu mwaka 2016 baada ya kushirikishwa na Mafikizolo kwenye ngoma yao 'Colour of Africa' wakiwa na Dj Maphorisa. Mwaka huohuo Diamond alimshirikisha, AKA kwenye ngoma yake Make Me Sing.
Diamond ni mmoja wa wasanii ambao ameutendea haki muziki wa Amapiamo kwa kutengeza hit nyingi kama Komasava (2024) akiwa na Jason Derulo ft Khalil Harisson & Chley, Shu (2023) akiwa na Chley. Mwaka 2021 Diamond aliachia IYO feat Focalistic, Mapara A Jazz & Ntosh Gazi na nyingine nyingi.
Diamond pia ameweza kufanya aina nyingine ya muziki ambayo ni Rhumba ambao asili yake ni Afrika ya Kati nchini Kongo. Kafanya na wasanii kama Fally Ipupa kwenye ngoma ya Inama (2019). Koffi Olomide kupitia ngoma yake Waah (2020), Papa Wemba kwenye ngoma yake ya 'Chacun pour soi' (2016) na Innoss'B Yope Remix (2019).
Aina nyingine ya muziki ambayo Diamond amefanya ni Hip-hop ambapo mwaka 2027 alishirikishwa na msanii wa muziki huo Fid Q kwenye remix ya wimbo wake wa Fresh akiwa na Rayvanny. Mduara kupitia nyimbo zake kama Kuna (2025), Nasema Nawe (2015) akiwa na Khadija Kopa. Lakini pia muziki wa Singeli kupitia ngoma yake ya Nitafanyaje iliyotoka (2025).

Leave a Reply