Siri jumba la Michael Jordan zaanikwa

Siri jumba la Michael Jordan zaanikwa

Michael Jordan, si jina geni masikioni mwa wengi. Hii ni kutokana na umahiri wake katika mchezo wa mpira wa kikapu NBA. Licha ya jina lake kuwa maarufu, wengi hawajui kuhusu siri zilizoko kwenye jumba lake la zamani lililouzwa mwishoni mwa mwaka 2024.

John Cooper, mzaliwa wa Nebraska, ambaye ndiye ni mmiliki halali wa sasa wa jumba hilo lenye futi za mraba 56,000 alilolinunua kwa takribani dola milioni 9.5. Kupitia mahojiano yake ameanika siri za kwenye jumba hilo.

Wakati akifanyiwa mahojiano na Daily Mail Cooper ameeleza kuwa wakati anaingia kwenye nyumba hiyo alikutana na vitu tofauti ambavyo vingine hajawahi kuvishuhudia katika maisha yake.



Kilichokuwamo ndani
Kwanza, anaeleza jumba hilo lina vitu vya kipekee ambavyo vinaonesha hadhi ya mchezaji maarufu, ikiwamo Nembo ya ‘Jumpman’ inayopatikana kwenye uwanja wa mpira wa ndani. Bendera za golf na hata thermostat ya kidijitali, pia kuna eneo la kuvutia sigara lenye humidor na meza za kadi, ambapo Michael Jordan alikuwa akipumzika.

Vitu vingine vinavyovutia ni pamoja na bwawa la kuogelea la infinity, uwanja wa golf, eneo la kuonywa mvinyo, na hata meza maalum iliyotengenezwa kwa mfano wa ramani ya mji wa Baghdad (mji mkuu wa Iraq). Huku wapenzi wa michezo wanaweza pia kucheza tenisi, pickleball au mpira wa kikapu.

Aidha, Cooper alifichukua kuwa alitumia zaidi ya miezi saba kufanya marekebisho katika jumba hilo na kuliweka kuwa na kiwango cha hali ya juu. Lakini alidai kuwa hakutaka kubadilisha kitu chochote alichokiweka Jordan. “Nataka kuheshimu urithi wa jumba hili,” anasema.

Kwa sasa, jumba hilo unaweza kulikodi katika mtandao wa Airbnb ambapo kwa wiki linapangishwa kwa dola 100,000 huku kwa mwezi ikiwa dola milioni 89,000. Ambapo kuna masharti kwa wapangaji kutoruhusiwa kupeleka wanyama na kufanya sherehe kubwa lakini pia ni lazima kutia saini mkataba wa kutochapisha habari za ndani katika mitandao ya kijamii.

Cooper anasema anatarajia kuendelea kumiliki jumba hili kwa muda mrefu, ingawa bado ana mipango mingine mikubwa ya marekebisho ambapo kwa sasa anasubiri kibali kutoka kwa mamlaka za mji wa Highland Park.

Michael Jordan ni mmoja wa wachezaji bora wa mpira wa kikapu duniani. Alizaliwa mwaka 1963 nchini Marekani na aliichezea timu ya Chicago Bulls katika Ligi ya NBA. Jordan alijulikana kwa ujuzi wake mkubwa, mbinu za kipekee na ushindi mwingi.



Alishinda mabao ya NBA mara 6 na kuwa MVP (Mchezaji Bora wa Msimu) mara 5. Alionekana katika michezo ya Olimpiki na kuisaidia Marekani kushinda medali za dhahabu. Jordan aliweka jumba hilo sokoni mwaka 2013, lakini halikuuzwa kwa miaka zaidi ya 10 kutokana na bei kuwa juu (akiuza dola milioni 29). Hatimaye, jumba hilo liliuzwa mwezi Desemba 2024 kwa dola milioni 9.5 kwa mwekezaji aitwaye John Cooper.

Hata hivyo sababu za kuuza jumba hilo zinatajwa kuwa kuhama hama kwa mchezaji huyo na kuishi sehemu mbalimbali hivyo hakuwa akilitumia jumba hilo mara kwa mara, huku sababu nyingine ikitajwa kuwa ni gharama kubwa za kulitunza jumba hilo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags