Fahamu kuhusu ugonjwa wa PID

Fahamu kuhusu ugonjwa wa PID

Hello vipenzi! Leo katika afya tumewasogezea mada nzuri sana kwa dada zetu, ugonjwa huo ambao unawasumbua baadhi ya wasichana lakini wanaona aibu kuweka wazi unafahamika kwa jina PID (Pelvic inflammatory disease). Leo tukujuza na kuelimisha ni jinsi gani utaweza kuepukana na ugonjwa huo.

Ugonjwa huu unafahamika kama PID ni maambukizi kwenye via vya uzazi wa mwanamke.

PID ni miongoni mwa magonjwa hatari sana kwa mwanamke, una madhara makubwa na unaambukizwa kwa njia ya kujamiiana.

Ugonjwa huu unaweza ukapelekea uharibifu mkubwa kwenye mfuko wa uzazi, mayai, mirija ya uzazi au sehemu nyingine za uzazi wa mwanamke

PID ni moja ya chanzo cha ugumba kwa mwanamke, kitu ambacho kinaweza kuzuilika.

TAKWIMU ZINAONESHA

Kila mwaka, zaidi ya wanawake milioni moja nchini Marekani wanapatwa na ugonjwa huu wa PID. Matokeo yake zaidi ya wanawake 100,000 wanakuwa wagumba kila mwaka.

Zaidi ya hayo, idadi kubwa ya mimba zaidi ya 100,000 inatungiwa kwenye mirija ya uzazi (ectopic pregnancy) inahusishwa na tatizo hilo la PID. Kiwango kikubwa cha maambukizi ni kwa wasichana wadogo. 

VIHATARISHI VYA UGONJWA WA PID

Maambukizi ya via vya uzazi vya mwanamke ni semi ya kitabibu inayoelezea maambukizi ya shingo ya uzazi, tumbo la uzazi na mirija ya fallopio. Kwa kawaida maambukizi haya husababishwa na bakteria.

Ingawa mara nyingi ni maambukizi yanayosambazwa kwa njia ya kujamiiana (STI), kama vile chlamydia au kisonono, wakati mwingine maambukizi haya huweza kusababishwa na bakteria wengine. PID inaweza kuwaathiri wanawake wenye umri wowote, lakini wale wenye umri kati ya miaka 15 and 24 huathirika zaidi.

 

VISABABISHI VYA PID

Kwa kawaida mlango wa uzazi (cervix) inazuia bakteria ambao wameingia ukeni wasisambae sehemu zingine za ndani za uzazi.

Kama mlango wa uzazi cervix umepatwa na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana kama kisonono au chlamydia, mlango huo wa uzazi unaathirika na unakuwa na uwezo mdogo wa kuzuia kusambaa kwa bakteria sehemu za ndani za uzazi.

PID inatokea pale vimelea vya magonjwa vinaposafiri kutoka kwenye mlango wa uzazi kwenda sehemu za juu za uzazi. Aslimia 90 ya PID husababishwa na kutotibiwa ugonjwa wa kisonono na klamidia.

Visababibishi vingine vya pid

  • Kutoa mimba
  • Kujifungua
  • Vipimo kwenye mlango wa uzazi 

DALILI ZA PID

 Zinatofautiana, zinaweza kuwa zifuatazo:

  • Maumivu ya tumbo sehemu ya chini au upande wa kulia
  • Kutokwa kwa uchafu ukeni usio wa kawaida wenye rangi ya kijani au ya njano na wakati mwingine una harufu isiyo ya kawaida
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu wakati wa tendo la ndoa
  • Maumivu wakati wa kukojoa
  • Maumivu sehemu ya kulia upande wa juu wa tumbo.

UTAMBUZI

Utambuzi mara nyingi huweza kufanywa kulingana na dalili na uchunguzi wa sehemu za siri. Wakati wa uchunguzi, sampuli za majimaji au usaha huchukuliwa ili kutambua bakteria anayesababisha maambukizi.

MAMBO YANAYOWEZA KUMUWEKA HATARINI MWANAMKE KUPATA PID

Kuna baadhi ya vitu ambavyo vinamuweka mwanamke katika hatari ya kupata PID ni kama vifuatavyo:

1.Wanawake wenye magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana kama kisonono na klaimidia wako hatarini sana kupata PID.

2.Wanawake ambao waliwahi kupata PID wako hatarini kupata tena.

  1. Wasichana wadogo wapo hatarini kupata PID kuliko wazee.

4.Wanawake wenye wapenzi wengi wako katika hatari ya kupata magonjwa ya zinaa na PID.

  1. Baadhi ya tafiti zinaeleza uoshaji wa uke unachangia kupata PID. Kuosha uke (douching) kunaweza pelekea kusukuma bakteria sehemu za juu za via vya uzazi na kuzuia kutoka kwa uchafu ambao mwanamke angeweza kutumia kama ishara ya kwenda kuonana na wataalamu wa afya mapema.

MADHARA YA PID

Kutokea /kujirudia kwa PID kunaweza kusababisha:

  • Kutokea kuharibika mirija ya uzazi
  • Ugumba
  • Mimba kutunga kwenye mirija ya uzazi (ectopic pregnancy)
  • Maumivu makali kwenye shingo ya kizazi

Kati ya wanawake nane (8) wanaougua PID, mmoja (1) anakuwa mgumba.

MATIBABU (PID TREATMENT)

Maambukizi ya via vya uzazi vya mwanamke hutibiwa kwa antibiotiki. Na tiba ya PID hutofautiana kulingana na ukali wa maambukizi. Ikiwa maambukizi ni makali, inaweza kuhitajika kupewa antibiotiki kupitia mishipa ya damu. Ikiwa maambukizi husababisha usaha kukusanyika au makovu kwenye mirija ya fallopio, basi upasuaji huweza kuhitajika ingawa hii ni nadra sana.

UBASHIRI

Watu wengi hupona vizuri baada ya matibabu na maambukizi hayasababishi matatizo ya muda mrefu. Hata hivyo, ikiwa maambukizi hayatatibiwa, au ikiwa mtu anayapata maambukizi haya tena baada ya kutibiwa, basi kuna uwezekano mkubwa wa kupata madhara zaidi. Haya huweza kujumuisha makovu kwenye tumbo la uzazi na mirija ya fallopio, ugumu wa kupata mimba, mimba kutungwa nje ya tumbo la uzazi na maumivu ya muda mrefu ya nyonga.

JINSI YA KUJIKINGA NA PID

PID inaweza kuzuilika kabisa, kisababishi kikubwa cha PID ni magonjwa ya zinaa, Mambo ya kuzingatia ili uweze kujikinga na PID ni:

  • Epuka kufanya mapenzi na watu wengi
  • Tumia njia za uzazi wa mpango kama kondomu
  • Tumia spermicides kwa kila tendo la ndoa hata kama unameza vidonge vya uzazi
  • Usitumie IUDs kama una wapenzi wengi.

NB: IUDs ni vitu vinavyowekwa ndani ya uke kuzuia mimba.

  • Wahi matibabu ukiona dalili zozote za PID au za magonjwa ya zinaa kama kutokwa na uchafu usio wa kawaida ukeni, maumivu kiunoni nk
  • Pia fanya uchunguzi wa afya ya uzazi mara kwa mara ili kama kuna tatizo ligundulike na litibiwe kabla halijasambaa kwenda kwenye viungo vya ndani vya uzazi.

Je unajihisi mgonjwa? Anza uchunguzi mapema.

Imeandaliwa na Mark Lewis






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post

Latest Tags