Mwigizaji kutoka Zanzibar Hemed Juma Jabu ‘Omary wa Kombolela’ ambaye ameonekana kwenye tamthilia kama Jivu, Shilingi na Kombolela ameeleza kinachokwamisha tasnia hiyo visiwani humo.
Akizungumza na Mwananchi Omary ameweka wazi kuwa moja ya sababu ni kutokuwa na soko la kununua filamu.
“Unguja hakuna wazalishaji wa filamu, kwa sababu hakuna soko la kununua kama ilivyo Dar es Salaam. Unguja Tv zipo lakini wanataka upeleke filamu bure waoneshe au wakupe elfu 20 ama 50 waoneshe filamu yako.
"Kiufupi Unguja hawaabudu sana mambo ya filamu. Labda ifunguliwe televisheni ya serikali itakayonunua filamu za Zanzibar tu, tena kwa kima ambacho wenzetu wanafanya. Ndio maana waigizaji wengi wa Zanzibar wanahamia Bongo kutafuta maisha mengine,” amesema
Akizungumza kuhusu Kombolela amesema hakutegemea kama atachanguliwa katika tamthilia hiyo ambayo kwa sasa imempa jina na heshima kubwa.
“Nikizungumzia kuhusu Kombolela ni tamthilia kubwa inayopendwa na kukubalika Afrika Mashariki. Namshukuru Mungu kuwepo kwenye tamthilia bora sikuwahi kutegemea. Lakini imekuwa kama surprise kwangu nimejisikia faraja mno kucheza kama Baba Sumaiya, nimecheza nafasi ndogo lakini nimeitendea haki.
"Ni tamthilia ambayo imeniongezea kitu kikubwa sana ikiwemo kufahamika na kupata mashabiki wapya. Kwa kweli sikutegemea kama ningekuwepo kwenye tamthilia hiyo. Nimshukuru Abdul Sanga (mwandishi wa Kombolela) kwa kunipa nafasi,Kombolela imeniongezea vitu vingi sana vingine siwezi kuvitaja hapa,” amesema Omary
Safari yake ya uigizaji ilipoanzia
“Safari yangu ya Sanaa nilianzia Zanzibar kiukweli kipindi hicho nilikuwa sijui kama nitakuja kuwa mwigizaji. Tulikuwa tunakusanya watu mtaani tunawafanyia maigizo wanacheka. Kwa Zanzibar kuna mida ile kuanzia saa 11 wanapenda sana kukaa vibarazani hivyo mimi na wenzangu tukawa tunatoa burudani kwa aina hiyo.
"Baada ya mama yangu kufariki ndugu zangu wakanichukua nikaja kuishi huku Dar es Salaam. Ndipo nikakutana na mshikaji wangu ambaye alinikutanisha na dada yake ambaye alikuwa anafanya mazoezi ya kuigiza katika kikundi cha ‘Ngome Entrertiment’, ambacho kilikuwa Mtongani kwa Aziz Ally. Ndipo nikapelekwa na safari yangu ikaanzia hapo ilikuwa ni mwaka 2009,” amesema Omary

Leave a Reply